Marekani yafanya mashambulizi mapya nchini Iran
26 Mei 2026
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani, CENTCOM, imesema mashambulizi hayo yalifanywa kwa ajili ya kujilinda dhidi ya vitisho vinavyotokana na vikosi vya Iran. Kwa mujibu wa msemaji wa kamandi hiyo Tim Hawkins, mashambulizi yalilenga maeneo ya kurushia makombora pamoja na boti zilizokuwa zikijaribu kuweka mabomu ya baharini.
Rubio asema mazungumzo na Iran yanaendelea
Mashambulizi hayo yamefanyika wakati wajumbe wa ngazi ya juu wa Iran walipowasili mjini Doha nchini Qatar kwa mazungumzo mapya yanayolenga kufikia makubaliano ya amani. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amesema mazungumzo yanaendelea na kwamba makubaliano bado yanawezekana, ingawa yanaendelea majadiliano ya kina kuhusu lugha na masharti ya rasimu ya awali ya makubaliano.
Iran haitaruhusiwa kuwa na silaha ya nyuklia
Rais Donald Trump pia amesema anaona maendeleo mazuri katika mazungumzo hayo. Hata hivyo amesisitiza kuwa Iran haitaruhusiwa kuwa na silaha za nyuklia na ametaka akiba ya urani iliyorutubishwa ya Iran iharibiwe au ikabidhiwe Marekani. Trump pia ametaka mataifa kadhaa ya Mashariki ya Kati kujiunga na Makubaliano ya Abraham ya kuhalalisha uhusiano na Israel kama sehemu ya mpango mpana wa amani.
Pezeshkian asema Iran haitashinikizwa
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema nchi yake haitasalimu amri mbele ya shinikizo la nje wala matakwa makubwa kupita kiasi. Amesema Iran itaendelea na diplomasia na mazungumzo, lakini kwa msingi wa kulinda haki na maslahi ya wananchi wake.
Hakuna uhakika wa kufikiwa makubaliano
Msimamo huo umekaririwa na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei ambaye amesema, licha ya mafanikio yaliyopatikana katika sehemu kubwa ya mazungumzo, bado hakuna uhakika wa kufikiwa makubaliano ya haraka kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya msimamo wa Marekani.
"Tunakabiliwa na misimamo tofauti na mara nyingi inayokinzana kutoka M arekani ndani ya muda wa saa chache tu, jambo ambalo linafanya mazungumzo kuwa magumu. Hata hivyo, tutachukua hatua kwa uthabiti katika diplomasia kama tulivyofanya vitani. Kwa macho wazi na kwa kuzingatia uzoefu wa awali, tutajitahidi kulinda maslahi ya taifa la Iran.”
Mashariki ya Kati haitalinda vituo vya Marekani
Kiongozi Mkuu wa Iran, amesema mataifa ya eneo la Mashariki ya Kati hayatakuwa tena ngao za kulinda vituo vya kijeshi vya Marekani.
Katika ujumbe wa maandishi uliorushwa na televisheni ya taifa kwa maadhimisho ya Sikukuu ya Eid al-Adha, Khamenei amesema Marekani haina tena maeneo salama ya kuendeleza kile alichokiita uchokozi wa kijeshi katika eneo hilo na kwamba ushawishi wake unaendelea kupungua siku baada ya siku.
Jeshi la Iran lasema lina haki ya kujilinda
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran limesema lina haki halali na ya moja kwa moja ya kujibu ukiukaji wowote wa usitishaji mapigano unaofanywa na Marekani. Jeshi hilo pia limedai kuwa limedungua droni ya Marekani aina ya MQ-9 na kufyatua risasi dhidi ya ndege ya kivita iliyoingia katika anga ya Iran.
Israel yazidisha mashambulizi yake Lebanon
Katika mzozo mwingine unaohusiana na huo, Israel imezidisha mashambulizi yake nchini Lebanon dhidi ya kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran. Mashambulizi ya anga katika Bonde la Bekaa yameripotiwa kuua watu 12, huku Israel ikiongeza wanajeshi katika eneo hilo.
Netanyahu aagiza mashambulizi dhidi ya Hezbollah
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema ameagiza kuongezwa kwa mashambulizi dhidi ya Hezbollah, wakati kundi hilo likiendelea kushambulia maeneo ya kaskazini mwa Israel kwa droni na makombora.
Mapigano hayo yanaendelea siku chache kabla ya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya wajumbe wa kijeshi wa Lebanon na Israel mjini Washington, huku matumaini ya amani yakikabiliwa na changamoto mpya katika eneo lote la Mashariki ya Kati.