1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yahakikisha mshirikiano na Korea Kusini

28 Juni 2018

Waziri wa ulinzi wa Marekani James Mattis ameihakikishia Korea Kusini kuhusu dhamira thabiti ya Marekani kuihakikishia usalama wake, ikiwemo kutopunguza idadi ya wanajeshi wa Marekani walioko nchini humo.

Südkorea USA James Mattis bei Song Young-moo in Seoul
Picha: Reuters/C. Sung-Jun

Waziri wa ulinzi wa Marekani James Mattis ameihakikishia Korea Kusini kuhusu dhamira thabiti ya Marekani kuihakikishia usalama wake, ikiwemo kutopunguza idadi ya wanajeshi wa Marekani walioko nchini humo, hata wakati wanadiplomasia wakitafuta makubaliano na Korea Kaskazini kuhusu kuachana na silaha zake za nyuklia. 

Kwenye ziara yake fupi nchini Korea Kusini, Mattis ametetea maamuzi ya rais Donald Trump aliyoyafanya mwezi huu ya kufuta mazoezi ya kijeshi na Korea Kusini, akisema huenda ikaongeza fursa kwa wanadiplomasia ya kufanya mazungumzo.

Mattis alikutana na waziri wa ulinzi wa Korea Kusini, Song Young-moo, alipozuru nchini humo kwa muda, akiwa njiani kuelekea Japan, wakati akitokea China. Ziara yake hiyo fupi ilibeba ujumbe uliolenga kuihakikishia Korea Kusini, baada ya Marekani kusitisha mazoezi ya pamoja ya kijeshi na nchi hiyo, yaliyopwangwa kufanyika baadae mwaka huu. Mattis alisema wajibu wa Marekani utahusisha pia kubakisha idadi ile ile ya wanajeshi wa Marekani waliopo sasa katika rasi ya Korea Kusini.

Trump alisitisha mazoezi ya kijeshi kati ya Korea Kusini na Marekani baada ya mkutano na Kim Jong UnPicha: Reuters

Marekani ina wanajeshi 28,500 nchini Korea Kusini. Rais Trump aliahirisha mazoezi hayo ya pamoja ya kijeshi, baada ya mkutano wa kilele na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un. Mwaka jana, mazoezi hayo yalihusisha wanajeshi 17,500 wa Marekani na zaidi ya wanajeshi 50,000 a Korea Kusini.

Kwa upande wake waziri wa ulinzi wa Korea Kusini, Song amesema mikutano tofauti iliyofanyika kati ya kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un na rais Trump na rais wa Korea Kusini, Moon Jae In imeweka msingi wa kufikiwa kwa makubaliano ya amani katika rasi hiyo ya Korea. 

Aidha mawaziri hao wawili kwa pamoja wamekubaliana kuhusu kubakia kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini, hadi pale taifa hilo litakapochukua hatua madhubuti za kuachana na mipango yake ya silaha za nyuklia. Lakini pia mawaziri hao wamekubaliana kutafuta hatua za ziada za kujenga uaminifu kati yao, wakati Korea Kaskazini ikiendeleza mazungumzo.

Mwandishi: Lilian Mtono/rtre/afp.

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW