Marekani yahimiza kupunguzwa mzozo kati ya Sudan na Ethiopia
6 Aprili 2021Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Ned Price, amesema katika mazungumzo yaliofanyika kupitia njia ya simu na Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok, Waziri Blinken amesisitiza umuhimu wa kupunguza mvutano kati ya Sudan na Ethiopia juu ya eneo la mpakani la Al-Fashaqa, ikiwemo makubaliano ya hivi karibuni ya kukaa pamoja na kutafuta suluhisho.
Eneo hilo linalogombaniwa na mataifa hayo mawili limeshuhudia ongezeko la machafuko wakati Sudan ikiwapeleka wanajeshi huko hatua ambayo Ethiopia imeielezea kama ya uvamizi.
soma zaidi: Serikali Ethiopia yashinikizwa kuondoa vikosi vyake Tigray
Eneo linalozozaniwa la Al-Fashaqa linapakana na jimbo la Tigray nchini Ethiopia, ambako serikali ya shirikisho ilianzisha operesheni dhidi ya uongozi wa jimbo hilo mwezi Novemba mwaka jana, na kusababisha takriban wakazi 60,000 kukimbilia katika nchi jirani ya Sudan.
Marekani ambayo ni mshirika wa muda mrefu wa Ethiopia imekuwa ikilikosoa taifa hilo ambapo Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken hivi karibuni alisema kile kinachoendelea Tigray ni mauaji ya kikabila.
Mzozo wa ujenzi wa bwawa la umeme la Ethiopia wajadiliwa
Uhusiano wa Marekani na Sudan ulianza pole pole kuimarika tangu Waziri Mkuu Hamdok kuchukua madaraka, katika serikali ya mpito kufuatia kuondolewa madarakani kiongozi wa muda mrefu Omar al Bashir.
Wiki iliyopita Sudan ilitoa milioni 335 kama fidia kwa serikali ya Marekani kufuatia mashambulio dhidi ya wamarekani wakati Bashir alipolitambua kundi la kigaidi la al qaeda.
Katika mazungumzo yake ya simu na Hamdok Blinken alizungumzia umuhimu wa kuanzia mazungumzo ya kidiplomasia kuhusu ujenzi wa bwawa la Ethiopia ambayo Addi Ababa inaendelea kuujenga licha ya pingamizi kutoka kwa Sudan na Misri wanaotegemea maji kutoka kwa mto Nile.
Marekani iliongoza majadiliano chini ya uongozi wa rais wa zamani Donald Trump kutafuta suluhisho. Umoja wa Falme za kiarabu UAE ni mpatanishi wa hivi karibuni katika mzozo huo.
Wiki iliyopita rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sissi alionya iwapo mfumo wake wa maji utaathirika kutokana na ujenzi wa bwawa hilo kutakuwa na majibu mabaya katika eneo hilo.
Chanzo: reuters