Marekani yaidhinisha chanjo ya pili ya COVID-19
19 Desemba 2020Marekani inakuwa taifa la kwanza kuidhinisha matumizi ya chanjo ya Moderna ambayo kama ilivyo ile ya Pfizer inatolewa mara mbili kwa mtu anayechanjwa.
Tayari imearifiwa kuwa mamilioni ya dozi yataanza kusafirishwa wikendi hii kutoka vituo vya hifadhi nje kidogo ya miji ya Memphis na Louisville.
Katika wakati Marekani inarikodi zaidi ya vifo 2,500 kwa siku kutokana na janga la virusi vya corona, vingozi waandamizi nchini humo ikiwemo makamu wa rais Mike Pence wamejitokeza kupatiwa chanjo jana Ijumaa.
Uamuzi wa Pence kupatiwa chanjo hadharani ni sehemu ya mpango mpana wa kuwashawishi wamarekani walio na shaka shaka juu ya usalama wa chanjo kujitokeza kwa wingi ili kupunguza kishindo cha janga la COVID-19 nchini humo.
Rais mteule wa Marekani Joe Biden, ambaye ataapishwa kuchukua hatamu za uongozi Januari 20, ametangaza kwamba atapatiwa chanjo hadharani Jumatatu inayokuja.
Rais Donald Trump anayekisiwa kuwa huenda anayo kinga dhidi ya virusi vya corona baada ya kupona COVID-19, ameashiria kuwa tayari kupatiwa chanjo.
Hapo Ijumaa Trump hakuonekana wakati Pence alipopatiwa chanjo, lakini amekuwa na shauku ya kuchukua ujiko kwa jinsi kampuni za Marekani zilivyoharakisha upatikanaji wa chanjo licha ya raia 310,000 kufariki dunia kutokana na COVID-19.
Mataifa mengi yanachukua hatua nzito kupunguza maambukizi
Mafanikio ya kupatikana chanjo ya pili yanakuja wakati serikali nyingi duniani zinazidisha mbinyo kwa kuwalazimisha watu kujitenga kuelekea sikukuu za Krismasi na mwaka mpya ili kupunguza kuongezeka kiwango cha maambukizi yatakayozidisha vifo mwanzoni mwa mwaka 2021.
Siku ya Ijumaa, Italia ilitangaza vizuizi vipya vikali vikiulenga msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka kwa kuamuru kufungwa kwa mikahawa, kumbi za starehe, safari kutoka jimbo moja hadi jingine na kila familia itaruhusiwa kufanya matembezi mara moja pekee kwa siku.
Nchini Australia, mji mkubwa wa Sydney, utaanza kutekeleza hatua mpya za kupiga marufuku shughuli za kawaida za umma kuanzia leo, huku viongozi wakitumai vizuizi hivyo vitasaidia kupunguza ongezeko kubwa la maambukizi mapya wakati wa msimu wa Krismasi.
Barani Ulaya, moja ya eneo lililoshambuliwa vibaya na janga la COVID-19, taharuki imeshamiri kufuatia waziri mkuu wa Slovakia Igor Matovic kubainika kuwa ameambukizwa virusi vya corona wiki moja tangu alipohudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels.
Mkutano huo unasadikiwa pia kuwa chanzo cha rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuambukizwa virusi vya corona. Maambukizi aliyoyapata Macron yamesababisha viongozi kadhaa wa Umoja wa Ulaya na serikali ya Ufaransa kuingia karantini.
Ulaya yakabiliwa na shinikizo
Umoja wa Ulaya ambao unaandamwa na shinikizo la kuidhinisha matumizi ya chanjo, unalenga kuanza kutoa chanjo ya Pfizer-BioNTech kabla ya mwisho wa mwaka, huku baadhi ya nchi wanachama zikitangaza Disemba 27 kuwa tarehe rasmi ya kuanza zoezi hilo.
Kwa upande mwingine, mataifa masikini duniani jana yalipata afueni baada ya Shirika la Afya Duniani na wadau wengine kutangaza kuwa chanjo zitaanza kusambazwa mapema mwaka unaokuja kwenye nchi 190 chini ya mkakati wa Covax uliobuniwa kuhakikisha chanjo za COVID-19 zinagawanywa kwa usawa kote duniani.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema "mwanga umeanza kuonekana"