1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaidhinisha mpango wa kuuokoa uchumi

24 Aprili 2020

Marekani imeidhinisha karibu dola nusu bilioni katika mpango mpya wa kuuokoa uchumi, wakati ulimwengu ukipambana na kutafuta mbinu za kuuokoa uchumi unaoathirika kwa janga la virusi vya corona.

Washington Kongress Abstimmung Coronavirus Finanzpaket Nancy Pelosi
Picha: Reuters/T. Brenner

Baraza la Wawakilishi Marekani limepitisha mswada mpya wa kichocheo cha uchumi wa dola bilioni 483 wakati kiwango cha ukosefu wa ajira kutokana virusi vya corona kikipanda na makampuni yakihitaji msaada zaidi. Mswada huo tayari ulikuwa umeidhinishwa na Baraza la Seneti, na Rais Donald Trump ameashiria kwamba atausaini haraka iwezekanavyo kuwa sheria. Mpango huo unaongeza kwa ule wa trilioni 2.2 ulioidhinishwa mwishoni mwa Machi.

Karibu watu 50,000 wamefariki dunia Marekani kutokana na virusi vya corona, huku idadi ya walioambukizwa ikifikia 866,646. Spika wa bunge Nancy Pelosi alisema mpango huo ni muhimu kwa kuzilinda familia za Marekani na kuhakikisha kuwa kampuni ndogo ndogo zina rasilimali zinazohitaji. "Dola bilioni 60 zitatengewa wanawake na jamii za walio wachache, maveterani, wamarekani asili, wanaoishi vijijini na watu ambao hawakuwa na fedha kwenye benki lakini wana mahitaji makubwa ya mikopo. Bilioni 60 nyingine ni mikopo na ruzuku kwa biashara ndogondogo. Na kisha dola bilioni 100 kwa mahospitali na upimaji."

Wabunge waliheshimu hatua za kuzuia maambukiziPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Harnik

Malumbano Ulaya

Barani Ulaya, ambalo ndilo lililoathirika pakubwa na vifo 110,000, viongozi wa Umoja wa Ulaya waliipa Halmashauri Kuu ya umoja huo jukumu la kutayarisha mpango wa kuufufua uchumi kwa ajili ya mporomoko unaotarajiwa, baada ya mazungumzo yaliyosifiwa kupiga hatua moja mbele, ijapokuwa wengine wameonya kuwa mazungumzo magumu bado yanakuja.

Aidha waliidhinisha mpango wa awali wa kipindi kifupi wa euro bilioni 540 na wakautaka mpango huo kuanza kufanya kazi mwanzoni mwa Juni.

Wakati ugonjwa huo ukionekana kuongezeka barani Ulaya na Marekani, mataifa mengine yangali katika hatua za mapema za vita hivyo ambavyo mpaka sasa vimewauwa Zaidi ya watu 190,000 na kuwaambukiza milioni 2.7 kote duniani.

Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO limeonya kuwa hatua kali zinapaswa kuendelea kutekelezwa hadi pale tiba mwafaka au chanjo vitakapopatikana.

Viongozi wa Ulaya walikuwa na mazungumzo makaliPicha: Getty Images/AFP/O. Hoslet

Juhudi zinaendelea kote duniani, huku Chuo Kikuu cha Oxford kikizindua majaribio ya chanjo kwa binaadamu. Ujerumani imetangaza kuwa majaribio ya aina hiyo yataanza wiki ijayo.

Katika Ikulu ya Marekani, wanasayansi wamesema wamegundua kuwa kirusi hicho kinaharibiwa haraka na miale ya jua, na kutoa matumaini kuwa janga hilo litapungua wakati msimu wa joto ukianza.

Baadhi ya nchi za Ulaya zimeanza kuondoa taratibu vizuizi vya kupambana na virusi vya corona, lakini marufuku dhidi ya mikusanyiko mikubwa imerefushwa. Migahawa, mabaa na matukio ya michezo bado vimefungwa.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametangaza kuwa serikali itaanza kuondoa vizuizi vilivyowekwa kuanzia Mei mosi. Ramaphosa amesema utaratibu huo utafanywa kwa umakini na tahadhari kubwa. Watu milioni 58 nchini Afrika Kusini wamefungiwa majumbani mwao kwa wiki tano, isipokuwa tu kama unataka kununua chakula au dawa. Nchi hiyo imerekodi viya 3,953 vya maambukizi na vifo 75

Vizuizi vilivyowekwa na serikali mbalimbali vitaathiri ulimwengu wa Kiislamu ambao hii leo unaanza mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW