Marekani yaikaripia Israel kuhusu ujenzi wa makaazi ya walowezi
1 Desemba 2012Mapema, Ikulu ya Marekani iliita hatua hiyo ambayo imekuja siku moja baada ya Umoja wa Mataifa kupiga kura ya kihistoria na kuipandisha Palestina hadhi ya nchi muangalizi siku ya Alhamisi kwa kuzingatia mipaka ya mwaka 1967, kama isiyo na manufaa yoyote. "Kwa kuzingatia tangazo la leo (30.11.2012), naomba nirejee kwamba utawala huu, kama tawala zilizotangulia, umeweka bayana kwa Israel kuwa shughuli hizo zinarudisha nyuma jitihada za majadiliano ya amani," alisema Clinton.
Clinton aliyasema hayo wakati akizungumza katika jukwaa lilioandaliwa na kituo cha sera za mashriki ya kati cha Saba mjini Washington, mbele ya hadhira iliyowajumuisha mawaziri wa mambo ya kigeni wa Israel Avigdor Lieberman na wa Ulinzi Ehud Barak. Clinton alisema kuwa suluhisho la kudumu la mgogoro wa Gaza lingekuwa mpango mpana wa amani kati ya Israel na Wapalestina wote, wakiongozwa na wawakilishi wao halali, mamlaka ya Palestina.
Aelezea sababu za kuipinga Palestina Umoja wa Mataifa
Utawala wa rais Barack Obama ulijaribu kuzuia shinikizo la Palestina la kutambuliwa na Umoja wa Mataifa, ukisema kuwa hatua hiyo ingekuwa kizingiti katika njia ya amani na kwamba taifa la Palestina lingetokana tu na mazungumzo na Israel. "Wote tunapaswa kuweka kituo baada ya kura ya wiki hii. Pande zote zinapaswa kutafakari kwa kina njia iliyoko mbele yetu," Clinton alisema. Aliongeza kuwa pande zote zinapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kutafuta njia ya kusonga mbele katika mazungumzo ambayo ndiyo yataleta suluhisho la mataifa mawili, ambayo inabaki kuwa shabaha yao.
Alisema pande mbili zitakapokuwa tayari kushiriki tena mazungumzo, rais Obama atakuwa tayari kushirikiana nao kikamilifu. Mapema, msemaji wa bazara la taifa la usalama, Tommy Vietor alisema kuwa Marekani inarejea upinzani wake wa muda mrefu dhidi ya makaazi ya walowezi, ujenzi mashariki mwa Jerusalem na matangazo ya Israel. "Tunaamini vitendo hivi havileti manufaa yoyote zaidi ya kuhujumu jitihada za kurudi kwenye meza ya mazungumzo;" alisema Vietor.
PLO yalaani tangazo la Israel
Taarifa za vyombo vya habari zimesema baadhi ya ujenzi wa Israel utafanyika katika eneo linalogombaniwa katika ukingo wa magharibi maarufu kama E1, ambalo linapita kati ya upande wa mwisho wa mashariki ya eneo lililotekwa la Jerusalem mashariki, na makaazi ya Maaleh Adumim. Chama cha Ukombozi wa Palestina, PLO, kimelaani hatua hiyo na kusema ni uvamizi dhidi ya taifa hilo. Wapalestina wanapinga kwa nguvu zote, mradi wa E1 kwa sababu unaligawanya eneo la ukingo wa magharibi katika vipande viwili - kaskazini na kusini, hatua ambayo inafanya uundwaji wa taifa la Palestina kuwa mgumu.
Wapalestina wanaitaka Jerusalem kuwa mji mkuu wa taifa lao na wanapinga mipango ya upanuzi wa Maaleh Adumim, eneo lililoko kilomita 5 kutoka ukingo wa mashariki wa mji wa Jerusalem. Kitendo cha Marekani kulaani ujenzi wa makaazi ya walowezi na Israel huko nyuma kimekuwa kikisababisha malumbano kati ya Obama na waziri mkuu Benjamin Netanyahu. Viongozi hao wawili wana uhusiano wa mashaka hivi sasa, licha ya hoja za utawala wa rais Obama kuwa serikali hiyo imefanya kazi ya ziada kuhakikisha inalinda usalama wa Israel kuliko utawala uliyopita.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Sekione Kitojo.