1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaikosoa Urusi kwa kuwaua raia Syria

Isaac Gamba30 Desemba 2015

Marekani imeikosoa Urusi kwa kuwaua mamia ya raia katika mashambulizi ya anga nchini Syria na pia kuishutumu kwa kuchangia kufifisha matumaini ya kusimamisha mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry.
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry.Picha: Reuters/M. Ngan

Hatua hiyo inakuja mnamo wakati matumaini ya Marekani yakielekezwa zaidi kwa Urusi katika kusaidia kuanzishwa mazungumzo ya amani kuhusiana na kumaliza mgogoro huo wa Syria hatua ambayo pia itayasaidia mataifa yote mawili kuelekeza nguvu zaidi katika kuliangamiza kundi la itikadi kali la dola la kiisilamu.

Mazungumzo kati ya wawakilishi wa serikali ya Rais Bashar al Assad na upande wa upinzani yanatarajiwa kuanza mwezi ujao ingawa bado kuna mambo hayajawekwa sawa katika hatua ya kuelekea kufanyika majadiliano hayo.

Makundi ya haki za binadamu nayo pia yamesema mashambulizi ya anga yanayofanywa na Urusi yanachangia kukuza mgogoro wa kibinadamu nchini humo kutokana na kusababisha mauaji ya raia ikiwa ni pamoja na kuwaacha mamilioni ya raia nchini humo bila ya makazi.

Waziri wa mambi ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei LavrovPicha: Reuters/M. Zmeyev

Kufuatia taarifa hizo za mauaji ya raia nchini Syria yanayosababishwa na mashambulizI yanayofanywa na Urusi pamoja na kutumia mabomu ya mtawanyiko, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry aliwasiliana na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergey Lavorov kumuelezea malalamiko yake kuhusiana na suala hilo. Hata hivyo maafisa wa Marekani hawakueleza jinsi waziri huyo wa mambo ya nchi wa Urusi alivyo yapokea malalamiko hayo.

Amnesty International yaonyesha vielelezo vya mashambulizi ya Urusi.

Aidha taarifa ya shirika la haki za binadamu - Amnesty International wiki iliyopita ilikuwa na vielelezo vinavyo onyesha Urusi inatumia mabomu ya mtawanyiko katika maeneo yenye wakazi wengi.Hata hivyo Urusi ilipinga madai hayo ikisema ni ya uongo.

Nembo ya shirika la Amnesty Internationa

Aidha Marekani imekiri kushuhudia ongezeko la taarifa zinazohusiana na idadi ya majeruhi tangu Urusi ilipoanzisha mashambulizi yake ya anga nchini Syria mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa Marekani Mark Toner alisema tathimini iliyokwisha fanywa inaonyesha kuwa mashambulizi ya mabomu ya Urusi nchini Syria yameonekana kutolenga kundi la itikadi kali la dola la kiisilamu na makundi mengine ya kigaidi kama Urusi inavyodai.

Toner amesema badala yake mashambulizi hayo mengi yamelenga maeneo yanayokaliwa na makundi ya upinzani dhidi ya utawala wa Rais Assad nchini humo ambako watu wengi wameuawa ama kujeruhiwa.

Mwandishi : Isaac Gamba/ APE

Mhariri :Hamidou Oummilkheir :

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW