1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaingiza mabilioni ya fedha katika mfumo wa mabenki kufuatia nchi za Ulaya kufanya hivyo.

Kitojo, Sekione14 Oktoba 2008

Rais wa Marekani ametangaza leo kuwa serikali yake itamimina kiasi cha dola bilioni 250 katika sekta ya benki nchini humo , kufuatia hatua kama hiyo iliyochukuliwa na mataifa ya Ulaya jana.

Rais Bush wa Marekani akitoa taarifa juu ya msukosuko wa fedha ulimwenguni kuhusiana na hatua ya kuyanusuru mabenki nchini humo.Picha: AP

Rais wa Marekani George W. Bush ametangaza leo Jumanne mipango ya serikali yake kumimina kiasi cha dola bilioni 250 katika sekta ya benki nchini humo, kufuatia hatua kama hiyo iliyochukuliwa na serikali za mataifa kadha ya Ulaya siku moja kabla.


Sekione Kitojo anaangalia hatua za mataifa kuingiza fedha katika mfumo wa mabenki ili kurejesha imani kwa wadau.



Lengo la mpango huo ni kufufua sekta hiyo ya fedha na kurejesha uchumi katika njia yake ya ukuaji, amesema rais Bush katika taarifa fupi aliyotoa kwa njia ya televisheni mjini Washington.

Ununuzi wa hisa na mitaji katika taasisi za benki zitakuwa ni hatua za muda mfupi, kuelekea uimarishaji masoko, Bush amesema.

Benki hapo baadaye zinaweza kununua tena mitaji yao na hisa kutoka serikalini.


Rais Bush ametahadharisha hata hivyo kuwa itachukua muda mrefu hadi pale athari za hatua zote za serikali kuelekea kuimarisha sekta hii ya fedha na uchumi kuweza kuonekana. Akitetea hatua hiyo ya kuingiza mabilioni ya fedha katika mfumo wa kifedha nchini Marekani, waziri wa fedha wa nchi hiyo Henry Paulson amesema.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya nchini Marekani , ununuzi huu wa serikali utajumuisha makampuni makubwa ya kifedha tisa ikiwa ni pamoja na Citi Group, benki ya Amerika na JP Morgan Chase. Shirika la utangazaji la CNBC limesema kuwa serikali inaweza kununua hadi benki zipatazo 1,000.

Tangazo la rais Bush linafuatia hatua iliyochukuliwa kwa pamoja na serikali za mataifa ya Ulaya jana Jumatatu kuingiza fedha nyingi ndani ya mfumo wa fedha ili kuipiga jeki sekta hiyo ya fedha. Kutokana na hatua hiyo masoko ya hisa duniani kote yalipanda kwa kiasi kikubwa jana Jumatatu, ambapo hali hiyo iliendelea hadi leo.

Uimarikaji wa soko la hisa la mjini London , Footsie, umeendelea katika mauzo ya leo kwa asilimia 4. Soko hilo la hisa limepanda kwa alama 157 na kufikia alama 4,413.9, lakini hisa za mabenki makubwa zimeendelea kuwa katika hali ya shaka shaka baada ya mpango wa uokozi uliotangazwa jana Jumatatu.

Hata hivyo soko kuu la hisa nchini China liliporomoka kwa karibu asilimia 3 leo Jumanne licha ya masoko mengi kupanda kutokana na hatua ya kuyaokoa mabenki. Soko la hisa la Shanghai Composite, ambalo linauza hisa kwa sarafu ya China na za kigeni , iliporomoka kwa asilimia 2.17 na kufunga soko hilo jana ikiwa na alama 2,017.32 ikiwa imekwenda chini kwa alama 56.25.

Biashara ilianza teana katika soko la hisa la Reykjavik leo baada ya siku tatu za kufungwa kabisa kwa soko hilo, ambapo liliporomoka kwa asilimia 76.13 wakati uchumi wa Iceland ukiendelea kukaribia ukingoni mwa kufilisika..