1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaiondolea vikwazo Iran kwa muda

22 Juni 2026

Kufuatia maendeleo kwenye mazungumzo ya amani nchini Uswisi, Marekani imetangaza kuiondolea Iran vikwazo vya mauzo ya mafuta kwa siku 60 zaidi hadi kufikia tarehe 21 Agosti 2026.

Uswisi Stansstad 2026 | JD Vance mazungumzo ya Marekani na Iran
Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance anasema kuna maendeleo mazuri kwenye mazungumzo ya amani na Iran.Picha: Nathan Howard/REUTERS

Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema mazungumzo ya amani na Iran yamejenga msingi wa kufikiwa mkataba wa mwisho wa kukomesha vita vilivyoanzishwa na nchi yake na Israel dhidi ya Iran mwishoni mwa mwezi Februari, huku upande wa ujumbe wa Iran kwenye mazungumzo hayo yaliyoanza jana nchini Uswisi ukisema masuala kadhaa yameanza kuonesha matumaini ya kutatuliwa.

Kwa mujibu wa Vance, mazungumzo  hayo kwenye hoteli ya kifakhari inayomilikiwa na Qatar nchini Uswisi yalianza vyema siku ya Jumapili (Juni 21), licha ya taarifa za awali kuashiria kwamba ujumbe wa Iran ulikuwa umetishia kujiondowa kupinga kauli ya Rais Donald Trump iliyotishia kuishambulia tena nchi yao.

Iran, ambayo imekuwa ikishikilia utekelezwaji kikamilifu ya makubaliano ya awali yaliyofikiwa wiki ijayo, hasa kipengele cha kusitishwa kwa uvamizi, ukaliaji na mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon, imeshuhudia leo hii ikiondolewa baadhi ya vikwazo vya uuzaji wa mafuta yake na wizara ya hazina ya Marekani. 

Muda mchache baada ya kumalizika kwa duru ya kwanza ya mazungumzo ya Uswisi, Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent, amesema nchi yake inaondowa kwa muda vikwazo dhidi ya Iran kwenye uzalishaji, uuzaji na ufikishaji wa mafuta ghafi na bidhaa zinazohusiana nayo hadi Agosti.

Fedha kununuwa maharage ya Marekani

Kwa mujibu wa kibali kilichochapishwa na wizara hiyo leo, mauzo na manunuzi yote yaliyokuwa yamepigwa marufuku yameruhusiwa kuendelea hadi majira ya saa sita na dakika moja mnamo tarehe 21 Agosti 2026.

Ujumbe wa Marekani na Pakistan kwenye mazungumzo ya amani na Iran nchini Uswisi.Picha: Government of Pakistan/Handout/Anadolu/picture alliance

Bessent amesema uamuzi huo unatokana na kukubali kwa Tehran kuendelea na mazungumzo ya kuufunguwa Mlango Bahari wa Hormuz  na kuwaruhusu waangalizi wa Shirika la Nguvu za Atomiki la Umoja wa Mataifa kuingia nchi humo kwa ukaguzi wa mradi wake ya nykulia.

Hata hivyo, wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kuondoka kurejea nyumbani, makamu huyo wa rais wa Marekani alisema fedha za Iran zinazoweza kuachiliwa kama mojawapo ya vipengele vya makubaliano ya awali, zitatumika kununuwa bidhaa za chakula kutoka kwa wakulima wa Marekani.

"Ikiwa kutakuwa na mali yoyote ya Iran itakayoachiliwa, basi tuna ridhaa ya mchakato huo. Waqatari wana ithibati kwa mchakato huo, na kisha fedha hiyo itanunuwa maharage, mahijnda na ngano kutoka kwa Wamarekani kwa wiki zijazo." Alisema Vance.

Kwa mujibu wa Vance, suala tete la vita vya Israel dhidi ya Lebanon nalo pia limepatiwa ufumbuzi wa awali kwa pande hizo mbili kukubaliana kuwa na utaratibu maalum wa kulishughulikia.

Pezeshkian kwenda Pakistan

Hayo yanajiri wakati Pakistan, mmojawapo wa wapatanishi wakuu wa mzozo huo, ikisema kuwa Rais Masoud Pezeshkian wa Iran anatazamiwa kuwasili Islamabad kwa ziara ya kikazi.

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran anatazamiwa kuwasili Islamabad nchini Pakistan siku ya Jumanne (Juni 22, 2026).Picha: Iran's Presidential website/WANA/REUTERS

Bila kufafanuwa zaidi, wizara ya mambo ya kigeni ya Pakistan imesema ziara hiyo ya Jumanne (Juni 23) "ni fursa muhimu ya kujadiliana mchakato wa kidiplomasia unaoendelea" kuelekea mkataba wa kudumu wa amani kati ya Washington na Tehran.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW