1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaisaidia Saudia Arabia kijeshi

21 Machi 2022

Katika majuma ya hivi karibuni Marekani imepeleka zana za kuzuia makombora Saudi Arabia, ikielezwa kuwa ni hatua yenye lengo la kupunguza mvutano unaotajwa kutatiza mahusiano baina ya mataifa hayo mawili washirika.

USA verlegen «Patriot»-Raketen von Deutschland nach Polen
Picha: Stringer/YONHAP NEWS/dpa/picture alliance

Usiku wa jana Jumapili, afisa mwandamizi katika serikali ya Marekani alithibitisha  kupelekwa kwa zana hizo. Afisa ambae alizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina lake kujadili uamuzi huo ambao haujatangazwa rasmi, alisema uamuzi huo unatokana na ahadi ya Rais Joe Biden ya azma ya kuwasaidia washirika wao katika eneo la Mashariki ya Kati.

Awali mshauri wa usalama wa taifa katika Ikulu ya Marekani, Jake Sullivan aliwalaani wapiganaji wa kundi la Houthi la Yemen baada ya kufanya mashambulizi kwa kutumia ndege zinazorushwa bila ya rubani na makombora dhidi ya vituo muhimu vya nishati vya Saudi Arabia, na kusababisha moto katika kituo kimoja wakati kituo kingine kikisitisha oparesheni zake za uzalishaji wa mafuta kwa muda.

Taarifa ya kuondolewa mfumo wa kujikinga na makombora Saudi Arabia

Rais wa Marekani, Joe BidenPicha: Tom Brenner/REUTERS

Mwezi Septemba, Shirikia la habari la "The Associated Press" liliripoti kwamba Marekani imeuondoa mfumo wake wa kujikinga na makombora ya Patriot kutoka katika kambi ya jeshi la anga ya Prince Sultan ambayo ipo nje ya mji wa Riyadh, pamoja na kwamba taifa hilo la kifalme likiendelea kukabiliwa na mashambulizi ya anga kutoka wa waasi wa Houthi wa Yemen. Saudi Arabia imesisitiza kwamba mfumo wa kujikinga ni muhimu kwa ulinzi wao dhidi ya makombora ya Houthi.

Taifa hilo lipo katika mkwamo wa kivita na waasi wa Houthi wenye kuungwa mkono na Iran, tangu mwaka 2015. Uamuzi wa  kuimarisha usambazaji nyenzo za kujikinga na makombora kwa mara ya kwanza uliripotiwa na jarida "Wall Street Journal."

Tuhuma za Marekani chanzo cha kuvurugika kwa uhusiano na Saudi Arabia

Uhusiano wa Marekani na Saudi Arabia ulianza kuzorota tangu Rais Biden aingiea madarakani. Rais huyo alikataa kufanya kazi moja kwa moja na Mwanamfalme Mohammed bin Salman na kadhalika kuliondoa kundi la Houthi katika orodha ya makundi ya kigaidi.

Mwaka uliopita serikali ya Biden ilitoa taarifa ya kijasusi, ambayo hitimisho lake lilionesha kuwa Mohamed bin Salman aliidhinisha kuuawa kwa mwandishi wa habari Jamal Khashoggimwaka 2018 katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul. Lakini kiongozi huyo alisisitiza kutohusika na tuhuma hizo.

Katika mahojiano yake ya hivi karibu na kituo kimoja cha televisheni, mrithi huyo wa ufalme wa Saudi Arabia aliulizwa, endapo Biden amepotoka jambo kumuhusu yeye. Alijibu kwa namna nyepesi kabisa, sijali na hilo ni juu yake Biden kufikiri.

Chanzo: AP

  

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW