1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaishambulia Iran, yenyewe yajibu mapigo

10 Juni 2026

Jeshi la Marekani limesema limekamilisha mashambulizi yake ya anga dhidi ya Iran kujibu kuangushwa kwa helikopta yake ambayo Rais Donald Trump amesema ilidunguliwa na Iran.

Marekani inasema imeishambulia Iran kwa kuangusha helikopta yake
Marekani inasema imeishambulia Iran kwa kuangusha helikopta yake. Picha: MCSN Dan Snow/Navy Office of Information/dpa/picture alliance

Jeshi la Marekani limesema limekamilisha mashambulizi yake ya anga dhidi ya Iran kujibu kuangushwa kwa helikopta yake ambayo Rais Donald Trump amesema ilidunguliwa na Iran. 

Taarifa ya Kamandi ya Jeshi la Marekani inayosimamia operesheni za eneo la mashariki ya kati, imesema vikosi vyake vimefanya mashambulizi na kuilenga mifumo ya ulinzi wa anga pamoja na rada za Irankatika na Mlango Bahari wa Hormuz. 

Iran nayo kwa upamde wake imesema imejibu hujuma hizo za Marekani kwa kufyetua droni na makombora kuzilenga kambi za jeshi la Marekani nchini Bahrain, Kuwait na Jordan. 

Kamandi ya jeshi la Marekani imeyataja mashambulizi iliyoyafanya kuwa ya "kiwango cha wastani kujibu uchokozi wa Iran,".

Vyombo vya habari vya Iran viliripoti milipuko kwenye kisiwa cha Qeshm na Mlango Bahari wa Hormuz, ujia muhimu wa usafirishaji mafuta ambao Iran iliufunga wakati wa vita.

Mashambulizi yanafuatia kauli ya Rais Donald Trump kuhusu kudunguliwa helikopta 

Rais Donald Trump wa Marekani.Picha: Al Bello/Getty Images/AFP

Rais Trump alisema hapo kabla kupitia andiko lake mtandaoni kwamba, Iran iliidungua helikopta ya jeshi la Marekani aina ya Apache iliyokuwa ikifanya doria kwenye eneo mlango bahari huo na akaapa kuwa Washington ilikuwa na wajibu wa kulipa kisasi kwa shambulio hilo.

Helikopta hiyo ni chombo cha pili cha anga cha jeshi la anga la Marekani ambacho Washington imekiri kuwa kimedunguliwa na Iran tangu kuanza kwa vita.

Mapema mwezi Aprili, Marekani ilipoteza ndege ya kivita chapa F15 iliyodunguliwa na Iran. Jeshi la Marekani limesema wanajeshi wake wawili walikuwemo kwenye helikopta hiyo waliokolewa karibu na pwani ya Oman.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran akaandika muda mchache baadaye kuwa vikosi vya nchi za kigeni vilivyopo kwenye eneo "vimo hatarini kila wakati" na kuonya kuwa jeshi la Iran halitokaa kimya iwapo nchi yao itashambuliwa.

Kwenye ujumbe wake kupitia mtandao wa kijamii wa X Abbas Araghchi alivitaka vikosi vya kigeni kuondoka kwenye kanda hiyo kama vinataka kuwa salama.

Iran yajibu mapigo kwa kuzilenga kambi za Marekani nchini Kuwait, Jordan na Bahrain

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran Abbas Araghchi.Picha: Khalil Hamra/AP Photo/picture alliance

Muda mchache baada ya kauli ya Araghchi, jeshi la Iran lilisema limeishambulia kwa droni kambi ya jeshi la Marekani nchini Bahrain kujibu mashambulizi ya Marekani. Limesema pia limevurumisha makombora kuelekea Jordan na Kuwait.

Kuangushwa kwa helikopta ya Marekani na mashambulizi ya Washington dhidi ya Iran na uamuzi wa Tehran kujibu mapigo, vyote hivyo vimeyatia doa makubaliano legelege ya kusitisha vita yaliyoanza miezi miwili iliyopita.

Hayo yametokea siku mojabaada ya Iran na Israel kushambuliana kwa mara ya kwanza tangu kusimamishwa kwa vita.

Katika hatua nyingine, jeshi la Israel limetoa amri ya watu kuondoka kwenye mji wa bandari kusini mwa Lebanon wa Tyre. Amri hiyo inawahusu pia jamii ndogo ya wakristo ambao hadi sasa maeneo yao kwenye mji huo hayakuwa yakishambuliwa na Israel.

Wiki iliyopita, Israel iliwaonya wakaazi Wakristo kuwa wapiganaji na wafuasi wa kundi la Hezbollah wamo miongoni mwao baada ya kukimbia mashambulizi makali kwenye maeneo ya karibu na mpaka wa nchi hizo mbili.

Licha ya madai hayo kupingwa, jeshi la Israel limesema litafanya operesheni kwenye maeneo yanayokaliwa na Wakristo na imewaamuru kuondoka.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW