Marekani yaishutumu Iran kuvuruga amani Mashariki ya Kati
30 Aprili 2018Katika ziara yake ya kwanza nje ya nchi saa kadhaa baada ya kuapishwa Mike Pompeo alikutana na viongozi wa Saudi Arabia na Israel nchi mbili ambazo zinamahusiano maalumu ya kimkakati na Marekani na ambazo pia zina adui wa pamoja Iran huku waziri mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu akisisitiza kuwa makubaliano ya nyukilia na Iran lazima yabadilishwe au yavunjwe ingawa mataifa mengi makubwa duniani yanayaona makubaliano hayo kuwa ndiyo njia inayoweza kuizuia Iran isiwe na silaha za nyukilia.
Akizungumza pembezoni mwa waziri mkuu wa Israel baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa masaa mawili mjini Telaviv waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alisema nia ya Iran kutaka kutawala siasa za Mashariki ya Kati bado ipo palepale na akasema hawatapuuza vitendo hivyo vya Iran kama ilivyokuwa kwa utawala uliotangulia.
Amesisitiza kuwa rais Donald Trump atajiondoa kwenye makubaliano ya nyukilia na Iran iwapo hayatafanyiwa mabadiliko huku waziri mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu akiongeza kuwa kiu ya Iran kutaka kutengeneza bomu la nyukilia lazima izuiwe ikiwa ni pamoja na uchokozi wake. Hata hivyo akizungumza kwa simu na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron rais wa Iran Hassan Rouhani amesema makubaliano ya nyukilia na Iran hayawezi kujadiliwa upya.
Netanyahu ampongeza Trump
Ama kwa upande mwingine waziri mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu amempongeza tena rais Donald Trump kwa uamuzi wake wa kutangaza kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel na kuwa wanasubiri kwa hamu kubwa kushuhudia utekelezaji wa hatua hiyo.
Katika mkutano na waandishi wa habari Mike Pompeo ameishutumu Iran kwa kuvuruga amani ya Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na kuunga mkono utawala wa kikatili wa rais wa Syria Bashar al- Assad pamoja na waasi wakishia nchini Yemen. Amesema Iran inayaunga mkono makundi ya kigaidi na pia kutoa silaha kwa waasi wa houthi nchini Yemen huku pia akiishutumu kwa kufanya kampeni za mashambulizi ya kimatandao.
Viongozi wa nchi zote mbili Saudi Arabia na Israel walionekana kufurahishwa na hatua ya Mike Pompeo kama ilivyo kuwa kwa Trump kuzijumuisha nchi hizo katika ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu ashike rasmi wadhifa huo.
Awali Mike Pompeo alikutana na mfalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdul-Aziz mjini Riyadhi baada ya hafla ya chakula cha jioni na mwana mfalme Mohamed bin Salman.
Akiwa Jordan mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani amekutana na mwenzake wa Jordan Ayman al -Safadi katika mji mkuu wa nchi hiyo ambapo viongozi hao mbali na kujadili mahusiano kati ya nchi hizo mbili, ametoa mwito pia kwa Palestina na Israel kurudi katika meza ya mazungumzo ya amani na kuongeza kuwa Marekani inaamini katika suluhisho la mataifa mawili huku pia ajenda ya kukutana na viongozi wa Palestina ikionekana kutokuwepo katika ziara yake hiyo ya Mashariki ya Kati mnamo wakati Palestina ikiishutumu Marekani kwa uamuzi wake wa kutangaza kuhamisha ubalozi wake kutoka mjini Tel Aviv na kuupeleka Jerusalem.
Hata hivyo aligusia vurugu ambazo zimekuwa zikitokea katika ukanda wa Gaza na kusema kuwa Marekani inaamini Israel ina haki pia ya kujilinda dhidi ya vurugu hizo. Ziara hiyo ya Mike Pompeo mashariki ya Kati inatarajiwa kukamilika leo.
Mwandishi: Isaac Gamba/afpe/DPAE/APE
Mhariri: Iddi Ssessanga