1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaitaka Taliban kusitisha mapigano

7 Mei 2020

Mjumbe wa Marekani kwa Afghanistan, katika mazungumzo mapya amelitaka kundi la Taliban kusitisha mapigano na kushikilia makubaliano ya miezi miwili yaliyotiwa saini na yanayolenga kumaliza vita va ya Afghanistan.

Zalmay Khalilzad
Picha: Reuters/O. Sobhani

Mjumbe huyo Zalmay Khalilzad ambaye alisimamia kutiwa saini makubaliano ya kusitisha mapigano ya Februari 29 na kundi la Taliban, alisafiri kuelekea Qatar hapo Jumanne, kwa huo mkutano mwengine, katika ziara itakayompelekea kupitia India na Pakistan.

Kulingana na Wizara ya Ulinzi ya Marekani, katika mikutano hiyo, Khalilzad ataunga mkono kusitishwa kwa mapigano mara moja, kuanza kwa haraka kwa mazungumzo baina ya wahusika wa mapigano Afghanistan na ushirikiano wa pande zote katika kukabiliana na janga la Covid-19 nchini Afghanistan.

Chini ya makubaliano na wapiganaji hao wa Kiislamu, Marekani imeanza kuondoa vikosi vyake kutoka Afghanistan kama sehemu ya mpango wa Rais Donald Trump wa kusitisha vita vya Marekani vilivyodumu kwa muda mrefu zaidi.

Taliban iliahidi kutofanya mashambulizi kwa vikosi vinavyoongozwa na Marekani

India imekuwa mojawapo ya nchi ambazo zina wasiwasi kuhusiana na Marekani kuondoa vikosi vyake ikihofia kwamba wanamgambo ambao ni mahasimu wa India watapata nguvu. Kwa upande wake Pakistan imefurahia makubaliano hayo.

Zalmay Khalilzad (kushoto) na Muasisi mwenza wa Taliban Mullah Abdul Ghani BaradarPicha: AFP/G. Cacace

Taliban iliahidi kwamba haitofanya mashambulizi dhidi ya vikosi kutoka muungano unaoongozwa na Marekani ila haikutoa ahadi kama hiyo kwa vikosi vya serikali ya Afghanistan.

Wiki iliyopita, Waziri wa nchi za kigeni wa Marekani Mike Pompeo alisema uongozi wa Taliban unafanya juhudi kubwa kupunguza mapigano.

"Marekani na Taliban kwa miongo kadhaa wamepitia kipindi cha uhasimu na kutoaminiana. Mazungumzo ya awali yalifeli. Juhudi hii ilikuwa kweli kwa Marekani pale Taliban ilipoonyesha ishara ya kutaka amani na kusitisha uhusiano wao na al-Qaeda na makundi mengine ya kigaidi," alisema Pompeo.

Pompeo pia alionekana kuikosoa serikali ya Rais Ashraf Ghani.

Subra ya Marekani kwa serikali ya Afghanistan inapwaya kila siku

Na sasa kumeripotiwa ongezeko la mapigano huku juhudi za kuwaleta wanamgambo hao na serikali ya Afghanistan inayotambulika kimataifa, katika meza ya mazungumzo, zikigonga mwamba.

Abdullah Abdullah (kushoto) na Ashraf Ghani (Kulia)Picha: picture-alliance/dpa/EPA/J. Jalali

Ni wazi kwamba subra ya Marekani kwa serikali ya Rais Ashraf Ghani inapungua kadri siku zinavyokwenda. Marekani haikumpongeza kwa kushinda muhula wa pili mwezi uliopita wakati ambapo kulikuwa na madai mengi ya wizi wa kura.

Ghani amepangiwa kuapishwa Jumatatu ijayo ila mpinzani wake mkuu Abdullah Abdullah ambaye anataka kuunda serikali hasimu ataapishwa siku hiyo hiyo. Na katika hali ambayo haikufikiriwa kwamba ingewahi kutokea, Marekani inaonekana kuwa tayari kutoishutumu Taliban kwa machafuko inayoendeleza na iisifu kwa vitendo hivyo badala yake.