1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaitaka Urusi kuheshimu makubaliano ya Minsk

Yusra Buwayhid
27 Februari 2017

Mapigano ya mashariki mwa Ukraine yamejeruhi wanajeshi kadhaa wa Ukraine, huku kikosi maalumu cha uangalizi Ukraine (SMM) cha Shirika la Usalama na Ushirikiano la Ulaya (OSCE) kikiwa kimewekewa vikwanzo.

Ukraine Zerstörung in Avdiivka | OSCE
Picha: Getty Images/AFP/A. Stepanov

Marekani imelaani shambulizi dhidi ya ujumbe maalum wa ufuatiliaji katika mashariki ya Ukraine na kutoa wito kwa Urusi na waasi wa upande wa Ukraine unaotaka kujitenga kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mjini Minsk. 

Katika taarifa yake, wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema inalaani mashambulizi dhidi ya kikosi maalumu cha uangalizi Ukraine (SMM) cha Shirika la Usalama na Ushirikiano la Ulaya (OSCE) pamoja na kukamatwa kwa nguvu kwa ndege isiyokuwa na rubani ya kikosi hicho.

"Marekani inaendelea kufuatilia kwa karibu vurugu zinazoendelea mashariki mwa Ukraine, pamoja na kushindwa kwa Urusi pamoja na waasi wanaotaka kujitenga, kuheshimu mkataba  wa kusitisha mapigano uliofikiwa miaka miwili iliyopita katika mji wa Minsk," amesema msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Mark Toner.

Taarifa hiyo ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeongeza kuwa lazima vikosi hivyo visitishe mashambulizi yake yanayoharibu miundombuni ya nchi, ikiwa ni pamoja na kituo cha kusafisha maji cha Donetsk. Urusi na waasi hao pia wametakiwa na Marekani kuondoa silaha zote nzito katika eneo hilo pamoja na kukisafishia njia kikosi maalumu cha uangalizi Ukraine cha Shirika la (OSCE).

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Mark TonerPicha: U.S. Department of State.

Mwito wa Marekani unakuja katika wakati ambapo kumezuka vurugu katika eneo hilo, huku Ukraine ikiripoti kuwa wanajeshi wake 16 wamejeruhiwa katika masaa 24 ya Jumamosi iliyopita.

Idadi hiyo ya majeruhi imekuja licha ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Urusi na Ukraine Jumatatu iliyopita. Wanajeshi wa Ukraine pamoja na waasi wamekuwa wakinyoosheana vidole vya lawama, kwa kushambuliana licha ya kuwepo kwa makubaliano ya amani.

Kikosi kinachojumuisha wanajeshi kutoka mataifa 57 cha shirika la OSCE, kimeripoti kupungua kwa kasi ya mapigano tokea kupatikana makubaliano hayo ya kusitisha mapambano. Lakini shirika hilo limesema, halina uhakika kama kweli pande zote mbili zimeweka silaha chini kama zilivyoahidi.

Mgogoro wa eneo la mashariki ya Ukraine, umesababisha vifo vya zaidi ya watu 10,000 tokea ulipoanza miaka mitatu iliyopita.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/afp/

Mhariri: Daniel Gakuba   

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW