Marekani yaituhumu Urusi kupeleka ndege za kivita nchi Libya
27 Mei 2020Katika tangazo lake lililochapishwa jana, kitengo cha jeshi la Marekani kinachohusika na bara la Afrika kikijulikana kwa kifupi kama Africom, kimesema ndege za kivita za Urusi zilitua kwanza nchini Syria ambako zilipakwa rangi upya kuficha asili ya nchi zinakotoka, na kisha zilisafiri hadi Libya. Africom yenye makao yake katika mji wa kusini mwa Ujerumani wa Stuttgart haikubainisha muda ndege hizo za Urusi zilipopelekwa Libya, ikisema tu kuwa ni hivi karibuni.
Msemaji wa makao makuu ya jeshi mjini Washington Jonathan Hoffman alisema Urusi ilipeleka ndege za kijeshi zipatazo 14 nchini Libya, zikiwemo kadhaa za chapa MiG-29 na SU-35. Picha zilizochapishwa na Africom kupitia mtandao wa Twitter zilizionyesha ndege hizo, ikisema zilikuwa zimesimama kwenye kituo kimoja cha anga.
Ikiwa taarifa hiyo ya jeshi la Marekani itathibitishwa, kupelekwa kwa ndege hizo za kivita za Urusi utakuwa ukiukaji mkubwa wa azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 2011, linalopiga marufuku uingizaji wa silaha nchini Libya.
Mamluki wa kirusi watimka kutoka Libya
Madai hayo ya Marekani yametolewa siku moja baada ya serikali ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa kusema kuwa mamia ya mamluki wa Urusi waliokuwa wakivisaidia vikosi vya kamanda Khalifa Haftar walikuwa wameondolewa kwenye uwanja wa mapambano kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.
Kuondolewa huko kunahusishwa na changamoto zinazoikabili operesheni ya mwaka mzima ya vikosi vya Haftar kutaka kuipokonya serikali ya Umoja wa kitaifa, udhibiti wa Tripoli.
Mara zote Urusi imekuwa ikikanusha kuhusika katika mzozo wa kivita nchini Libya, na wizara yake ya ulinzi imesema haiwezi kusema chochote kuhusu madai ya Africom, lakini mbunge mmoja ambaye ni mjumbe wa kamati ya Ulinzi amesema taarifa hizo za jeshi la Marekani ni uzushi mtupu.
Urusi yasema inaunga mkono mazungumzo
Huku hayo yakiarifiwa, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov amemuarifu kamanda Khalifa Haftar, kwamba Urusi inaunga mkono usitishwaji wa mapigano nchini Libya, na pia mazungumzo ya kutafuta suluhisho la kisiasa litakalowezesha kuundwa kwa utawala wa umoja wa kitaifa.
Kwa mujibu wa tangazo la wizara ya mambo ya nje mjini Moscow, ujumbe huo wa njia ya simu ulipitishwa kwa Aguila Saleh Issa, spika wa Baraza la Wawakilishi la Libya lenye makao yake katika mji wa mashariki wa Tobruk, ambaye ni mshirika wa karibu wa Khalifa Haftar.
afpe, rtre