1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaiwekea tena Iran vikwazo

7 Agosti 2018

Awamu mbili za kwanza za vikwazo vya Marekani kwa Iran zimeaanza kutekelezwa leo. Vikwazo hivyo vinalenga kuizuia Iran kununua dola za Marekani na pia vinalenga viwanda muhimu.

Iran Sanctions Hassan Rouhani
Picha: picture-alliance/AP Photo/Iranian Presidency Office

Marekani imeiwekea tena Iran vikwazo, na kurudisha adhabu kali ambazo ziliondolewa kufuatia mkataba wa kihistoria wa nyuklia ambao rais Donald Trump aliachana nao mwezi Mei. Wakati huohuo, Iran imeilaumu Marekani kwa kuendeleza vita vya kisaikolojia. Kwa upande mwingine sheria ya Umoja wa Ulaya ya kulinda kampuni zake zinazofanya biashara na Iran dhidi ya athari za vikwazo vya Marekani imeanza kutekelezwa.

Awamu mbili za kwanza za vikwazo hivyo vya Marekani kwa Iran zimeaanza kutekelezwa leo, zikilenga kuzuia Iran kununua dola za Marekani na pia kulenga viwanda muhimu vikiwemo vya magari na mazulia.

Trump alisema yuko tayari kwa mazungumzo na Iran ili kupata mkataba mpya utakaoshughulikia masuala yote yenye utata. Lakini rais wa Iran Hassan Rouhani amesema Marekani inataka kuanzisha vita vya kisaikolojia dhidi ya Iran. Ameeleza kuwa hakuna maana kufanya mazungumzo wakati kuna vikwazo. "Wanataka kuanzisha vita vya kisaikolojia dhidi ya taifa la Iran na kusababisha migawanyiko miongoni mwa watu. Lengo lake ni kunufaika katika uchaguzi ujao wa ubunge hivi karibuni.”

Trump ashikilia msimamo kuwa mkataba wa Iran kuhusu nyuklia ni mbaya sana

Rais wa Marekani Donald Trump akizungumza na waandishi habari baada ya kusaini amri ya kuiwekea iran vikwazoPicha: Reuters/J. Ernst

Kwenye amri yake hapo jana, Trump alisema vikwazo hivyo vinanuia kuiwekea Iran shinikizo kifedha, ili kulazimisha suluhisho pana na la kudumu kwa vitisho vya Iran, ikiwemo utengenezaji wake wa makombora na shughuli zake za udhoofishaji wa kikanda.

Kwa mara nyingine Trump aliutaja mkataba huo kuwa mbaya sana, unaoegemea upande mmoja na ulioshindwa kutimiza malengo ya kimsingi ya kuziba njia zote kwa Iran kumiliki mabomu ya kinyuklia.

Marekani ilijiondoa kwenye mkataba huo licha ya wadau wengine kwenye muafaka huo ambao ni Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Umoja wa Ulaya kumsihi Trump kutojiondoa kwenye mkataba huo unaolenga kuizuia Iran kumiliki silaha za nyuklia. Hali iliyoangazia mbinu ya Trump ya kufanya mambo kivyake na tabia yake ya kutoheshimu makubaliano ya pamoja.

Umoja wa Ulaya kuanza kulinda kampuni zinazofanya biashara na Iran dhidi ya athari za vikwazo

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini akihudhuria mkutano wa mawaziri Vienna kuhusu mkataba wa Iran wa nyukliaPicha: Getty Images/AFP/H. Punz

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema umoja huo sawa na Uingereza, Ujerumani na Ufaransa zimesikitishwa mno na hatua ya Marekani.

Kupitia taarifa, Mogherini amesema wamejitolea kulinda wadau wa kiuchumi wanaofanya biashara halali na Iran. Hapo jana Umoja huo ulisema utaanza kutekeleza sheria inayozilinda kampuni za Ulaya dhidi ya vikwazo vya Marekani kwa Iran. Msemaji wa Umoja wa Ulaya Mina Andreeva anaeleza: "Sheria ya Umoja wa Ulaya iliyoimarishwa ya kulinda kampuni za Umoja wa Ulaya zinazofanya biashara halali na Iran inaanza kufanya kazi kuzilinda dhidi ya vikwazo vya marekani.”

Tayari Iran imeanza kushuhudia athari za kikwazo hivyo, huku sarafu ya Iran rial ikipoteza takriban nusu ya thamani yake, tangu Rais Trump alipotangaza Marekani itajiondoa kwenye mkataba wa mwaka 2015.

Athari za kurudishwa kwa vikwazo hivyo zimezusha taharuki kwa Iran ambayo imekumbwa na maandamano ya siku kadhaa na migomo katika miji mingi kuhusu uhaba wa maji, bei ya juu za bidhaa na ghadhabu kuhusu mfumo wao wa kisiasa.

 

Mhariri: Zainab Aziz

     

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW