1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaiwekea vikwazo kampuni ya programu ya Pegasus

4 Novemba 2021

Marekani imeiweka kampuni ya Israel inayotengeneza programu ya udukuzi ya Pegasus katika orodha ya makampuni mabaya kufuatia sakata la kuwachunguza waandishi habari na maafisa wakuu serikalini.

Israel | NSO Group
Picha: Jack Guez/AFP/Getty Iamges

Kampuni hiyo ya Israel ya NSO iliingia mashakani baada ya ripoti kutolewa kwamba maelfu ya wanaharakati wa kutetea haki za binaadamu, waandishi habari, wanasiasa na wakurugenzi wa biashara kubwa kubwa duniani waliorodheshwa kama watu wanaolengwa katika programu ya Pegasus.

Simu za mkononi zilizoathirika kwa programu hiyo, zimetumika kuwachunguza watu tofauti kwa kusoma jumbe zinazoingia, kuangalia picha zao, kufuatilia mienendo yao na hata kuwasha kamera zao bila wao kujua.

Idara ya ufuatiliaji wa data nchini Marekani imesema katika taarifa yake kwamba programu za ujasusi zinaziwezesha serikali za kigeni kufanya ukandamizaji, ambao kwa kawaida hufanywa na serikali zinazoongoza kimabavu kwa wapinzani wake, waandishi habari na wanaharakati nje ya mipaka yao yanayolenga kuwanyamazisha.

soma zaidi: Ufichuzi kuhusu Pagasus na kashfa kubwa ya udukuzi

Hata hivyo kampuni ya NSO imesema teknolojia zake zinaunga mkono masilahi ya usalama wa kitaifa wa Marekani pamoja na sera kwa kuzuwiya ugaidi na uhalifu. Msemaji wa kampuni hiyo amesema wanafuatilia kujaribu kuona uamuzi uliochukuliwa na Marekani unabatilishwa.

Marekani pia imeiorodhesha kampuni ya Israel ya Candiru, kampuni ya usalama wa Kompyuta ya PTE (COSEINC) pamoja na kampuni ya Urusi ya Positive Technologies kama kampuni zilizotumiwa kuuza vifaa vya kufanyia udukuzi.

kampuni ya Positive Technologies yasema hatua ya Marekani haijawashitua

Kuongezwa kwa kampuni hizo katika orodha ya makampuni mabaya, kunamaanisha ni marufuku kwao kupokea vifaa vya aina yoyote kutoka kwa mashirika ya Marekani na itakuwa vigumu kwa watafiti wa Marekani kuwauzia habari zozote au hata teknolojia.

Kwa upande wake, kampuni ya Positive Technologies imesema hatua ya kuiweka katika orodha hiyo haikuwashangaza lakini pia haitoiathiri. Imesema itaendelea kufanya kila iwezalo kuhakikisha usalama wa mtandaoni unaimarishwa. Nayo kampuni ya COSEINC bado haijatoa tamko kuhusiana na hatua hiyo iliyochukuliwa na Marekani.

Kwa sasa wataalamu wa Umoja wa Mataifa wametoa wito wa kuzuiwa kuuzwa kwa programu za udukuzi hadi pale kanuni zitakapowekwa ili kulinda haki za binaadamu kufuatia kashfa ya Pegasus.

Kando na wasiwasi uliopo juu ya programu hiyo, kumeibuka wimbi jengine la hofu wakati kampuni ya kutengeneza iPhone Apple  ilipozungumzia hitilafu mwezi Septemba kwamba programu za udukuzi huenda zikaathiri vifaa hivyo bila hata ya mtumiaji kubonyeza kiungo kitakachokuwa kimetumwa katika simu yake.

Chanzo: afp

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW