1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yajaribu kutuliza wasiwasi Mexico

24 Februari 2017

Maafisa wa Marekani wameihakikishia Mexico kuwa hakutakuwa na ufukuzwaji wa kimakundi au kulitumia jeshi la Marekani kuwatimuwa wahamiaji haramu, walioelezwa na Rais Donald Trump kuwa watu waovu.

Mexiko US-Außenminister Tillerson auf Besuch mit Amtskollegen Videgaray
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson akisalimia na mwenzi wake wa Mexico Luis Videgaray.Picha: Reuters/C. Jasso

Mawaziri wa Marekani - wa mambo ya ndani John Kelly na wa nje Rex Tillerson walikutana na mawaziri wa Mexico walioeleza wasiwasi na kukerwa na msimamo wa kibabe wa Trump kuhusu uhusiano wa kibiashara na uhamiaji na Mexico.

Waziri wa mambo ya nje wa Mexico Luis Videgaray alisema baada ya kukutana na mawaziri Kelly na Tillerson kwamba serikali za mataifa hayo zimechukua hatua muhimu kuelekea njia sahihi. Uhusiano kati ya Marekani na Mexico umekuwa wa mvutano tangu kuapishwa mwezi Januari kwa Donald Trump, ambaye ameapa kukomesha uhamiaji haramu kutoka Mexico.

Sheria kuzingatiwa kufukuza wahamiaji haramu

Wizara ya usalama wa ndani ilitoa maagizo mapya siku ya Jumanne, kuimarisha ukamataji na urejeshwaji wa wahamiaji haramu, wengi wao wakiwa raia wa Mexico. Lakini waziri Kelly aliahidi katika mkutano wa habari mjini Mexico City siku ya Alhamisi, kwamba hakutakuwa na urejeshwaji wa makundi ya watu.

(Kushoto - Kulia) Waziri wa usalama wa ndani wa Marekani John Kelly, waziri wa mambo ya nje wa Mexico Luis Videgaray na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson baada ya kuhutubia mkutano wa pamoja na waandishi habari.Picha: Getty Images/AFP/R. Schemidt

"Hakutakuwepo, na narudia, hakuna kufukuza watu kimakundi. Kila kitu tunachokifanya katika wizara ya usalama wa ndani kitafanywa kisheria, na kuzingatia haki za binadamu katika mfumo wa sheria wa Marekani. Urejeshaji wote utafuata mfumo wetu wa sheria," alisema Kelly katika mkutano na waandishi habari mjini Mexico City.

Akizungumza mapema katika ikulu ya White House, Trump aliuelezea urejeshaji wa makundi ya wahamiaji kuwa operesheni ya kijeshi. Lakini Msemaji wake Sean Spicer baadae akauambia mkutano wa waandishi habari kwamba Trump alikuwa akitumia neno "jeshi" kama kivumishi kumaanisha ufanisi. Au kama Tump mwenye alivyoeleza: Tunawafukuza watu waovu nchini mwetu, na kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.

Ujenzi wa ukuta mpakani

Janauri 25, Trump alisaini Amri ya Rais ya kuanza mara moja ujenzi wa ukuta kwenye mpaka wa kusini, wakati ambapo waziri Luis Videgaray alikuwa akiongoza ujumbe wa Mexico kuelekea mjini Washington. Madai ya Trump kwamba Mexico italipia ujenzi wa ukuta huo yalisababisha kufutwa kwa ziara ya rais wa Mexico Enrique Pena Nieto katika ikulu ya White House.

Trump pia ameahidi kuujadili upya mkataba wa biashara huru wa mataifa ya Amerika Kaskazini NAFTA, pamoja na Canada na Mexico, akiulaumu mkataba huo huo wa miaka 23 kwa kuchangia kwa sehemu kutoweka kwa ajira katika sekta ya viwanda ya Marekani.

Rais wa Marekani Donald Trump amesababisha mtikisiko mkubwa nchini Mexico tangu alipoingia madrakani Januari 20, 2017.Picha: Reuters/J. Ernst

Tillerson na Kelly baadae walikutana na Rais Pena Nieto, baada ya kukutana na waziri wa mambo ya nje Videgeray pamoja na mawaziri wa mambo ya ndani Miguel Osorio Chong, na waziri wa fedha wa Mexico Jose Antonio Meade. Tillerson alisema baada ya mazungumzo ya mawaziri kwamba Marekani na Mexico zinaunganishwa na dhamira ya pamoja ya kuheshimiwa kwa sheria na taratibu kwenye mpaka wao wa pamoja.

Wakati huo huo, watu kadhaa wengi wao wakiwa Wamarekani waliandamana mbele ya ubalozi wa Marekani wakitaka kusitishwa kwa vita vya maneno vya Trump dhidi ya Mexico. Katika hatua ambayo yumkini imelenga kuitia kishindo zaidi Mexico, Trump ameyagisha mashirika ya serikali ya Marekani kuhesabu ni misaada kiasi gani wanatoa kwa nchi hiyo.

Pia ameahidi kuziadhibu kampuni za Marekani zinazozalisha bidhaa zake nchini Mexico, na ametishia kuzuwia marejesho ya fedha za Wamexico wanaofanya kazi Marekani.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe, dpae,

Mhariri: Saumu Yusuf

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW