1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yajitoa rasmi mkataba wa tabia nchi wa Paris

4 Novemba 2020

Marekani imejiondoa rasmi kwenye makubaliano ya Paris ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, yaliyosainiwa 2015. Ushiriki wake katika makubaliano hayo katika siku zijazo utategemea matokeo ya uchaguzi wa rais

Klimakonferenz Cop21 2015 in Paris
Picha: picture-alliance/AA/A. Bouissou

Kwa Marekani, muda wa mwaka mmoja ambao kila nchi inayojitoa katika makubaliano hayo ya kimataifa, inahitajika kusubiri baada ya kutangaza nia yake ndipo ijitoe, umemalizika leo.

Utawala wa Donald Trump uliujulisha Umoja wa Mataifa mwaka uliopita, nia ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano hayo.

Kwa kujitoa rasmi leo, Marekani imekuwa taifa la kwanza ulimwenguni kujiondoa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa yanayolenga kupambana na utoaji wa gesi zinazochafua mazingira pamoja na athari nyinginezo za mabadiliko ya tabia nchi. Uwezekano wa Marekani kujihusisha tena na makubaliano hayo katika siku zijazo, utategemea pakubwa matokeo ya uchaguzi wa rais.

Rais Trump anashikilia kwamba Marekani iwe nje ya mkataba huo, lakini mshindani wake Joe Biden, anataka kuirudisha Marekani kwenye mkataba huo. Ina maana ikiwa Trump atachaguliwa tena, basi Marekani ambayo ni taifa lenye uchumi mkubwa zaidi ulimwenguni na la pili katika uchafuzi wa mazingira baada ya China, litaendelea kuwa nje ya mkataba huo.

Trump alitangaza kuiondoa Marekani katika mkataba huoPicha: Reuters/J. Ernst

Katika muhula wake wa kwanza akiwa madarakani, Rais Trump ametilia mashaka mitizamo mingi ya kisayansi kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, msimamo unaochochewa na nishati ya visukuku pamoja na kudhoofika kwa ulinzi wa mazingira. Trump amekuwa mpinzani mkali wa makubaliano hayo, na amefuta sheria kadhaa za mazingira, akisema zinazuwia biashara na kuyapa faida mataifa mengine.

Hatua hiyo imeuweka utawala wake kwenye mzozo na washirika wake pamoja na washindani wake wakuu. Lakini Joe Biden ameapa kuirudisha Marekani katika mkataba huo ikiwa atashinda urais. Biden ametaja mabadiliko ya tabia nchi pamoja na ongezeko la joto ulimwenguni kama kitisho kilichopo kwa binadamu na kwamba Marekani inayo wajibu wa kukishughulikia kitisho hicho.

Biden amependekeza mpango wa bajeti ya dola trilioni 1.7 ili kupunguza kabisa utoaji wa gesi chafu nchini Marekani hadi asilimia sifuri kufikia mwaka 2050. Hata hivyo kwa sasa, haijalishi namna ambavyo matokeo yatakavyokwenda. Lililo wazi ni kwamba Marekani itakuwa nje ya mazungumzo wakati Uingereza na Umoja wa Mataifa watakapokuwa wenyeji wa mkutano wa kilele Desemba 12, kuhusu Tabia nchi. Mkutano huo utakuwa pia maadhimisho ya miaka mitano ya makubaliano hayo ya Paris.

Wanasayansi kuhusu mabadiliko ya tabia nchi wameonya kuwa endapo hatua hazitachukuliwa kwa dharura, basi ongezeko la joto duniani litapindukia nyuzijoto 2, zaidi ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda. Hali ambayo, itasababisha misururu ya majanga kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ifikapo mwisho wa karne hii.

Ni Vipi tunaweza kuondoa gesi ukaa katika mazingira?

Hali hii inaweza kuepushwa ikiwa utoaji wa gesi zinazochafua mazingira duniani utapunguzwa kabisa ifikapo katikati ya karne. Hayo ni kulingana na jopo la Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi. Mnamo Jumanne, Niklas Hohne ambaye ni mwanasayanzi kuhusu tabia nchi kutoka Uholanzi, aliunga mkono mpango wa Joe Biden. Kwenye ukurasa wake wa Twitter aliandika ''Uchaguzi huu unaweza kuwa wa kujenga au kuvunja kuhusu sera ya kimataifa kuhusu tabia nchi. Mpango wa Biden pekee unaweza kupunguza ongezeko la joto kwa nyuzijoto 0.1. kila moja juu ya kumi ni muhimu.''

(DW)