Marekani yakabidhi jimbo la Anbar kwa serikali ya Iraq
1 Septemba 2008Jimbo la Anbar ni jimbo la 11 kuwajibika wenyewe na shughuli za usalama.
Sherehe za kijeshi zimeadhimisha kukabidhiwa huko huku usalama ukiwa wa hali ya juu.
Meja Generali John Kelly kamanda wa vikosi vya Marekani huko Anbar amewaambia maafisa wa Marekani Iraq na wale wa kikabila waliokusanyika karibu na makao makuu ya serikali ya Anbar kwamba wako katika hatua za mwisho za mapigano mabaya kabisa na kwamba lengo liko wazi kuwa maisha yao na maisha ya watoto wao yanategemea ushindi.
Kelly na Gavana wa Anbar Mamun Sami Rasheed walikumbatiana baada ya kusaini waraka wenye kuifanya Anbar kuwa jimbo la 11 kati ya majimbo 18 ya Iraq na jimbo la kwanza la Masunni kurudishwa kwa udhibiti wa Iraq tokea uvamizi wa nchi hiyo uliongozwa na Marekani hapo mwaka 2003 kumn'gowa Saddam Hussein.
Rasheed amekaririwa akisema wamekabiliana na Al Qaeda na kwa ajili hiyo wamepoteza maisha ya watu wao wengi kwamba damu imemwagika katika ardhi hiyo adhimu.
Polisi ilipiga gwaride katika bararaba kuu wakibeba bendera za Iraq wakifuatiwa na gwaride la magari ya polisi yaliokuwa yamepambwa mauwa.
Anbar ina tajiri mdogo wa mafuta lakini muhimu kutokana na mipaka yake na Syria,Saudi Arabia na Jordan hapo zamani ilikuwa pepo kwa Waislamu wa itikadi kali wa kundi la Al Qaeda na mahala pa mapambao makali dhidi ya vikosi vya Marekani na serikali ya Iraq inayoongozwa na Mashia.
Mojawapo ya mapigano makali kabisa katika kipindi cha vita cha zaidi ya miaka mitano yametokea Anbar ikiwa ni pamoja na mashambaulizi makubwa ya Marekani kwa mji wa Falluja hapo mwaka 2004.
Mapigano ya kwanza inaaminika kuwa yaliua mami ya raia na yale ya pili yaliharibu sehemu kubwa za mji huo na kuziwacha kuwa magofu.
Sehemu kuu za mji huo awali zilikuwa chini ya udhibiti wa kundi la Al Qaeda.
Mshauri wa usalama wa taifa nchini Iraq Mowaffaq al Rubaie amewaambia waandishi wa habari kwamba kati walikuwa hawakuwaza hayo katika matumaini yao miaka mitatu au minne iliopita na kwamba wangelisema watakabidhi mamlaka ya kiraia majukumu ya usalama kutoka kwa vikosi vya kigeni watu wangeliwacheka lakini leo hii jambo hilo limekuwa la kweli.
Mambo yalibadilika huko Anbar mwishoni mwa mwaka 2006 wakati viongozi wa makabila ya Kisunni waliochoshwa na mbinu za kikatili za Al Qaeda walipobadili msimamo na kuamuwa kusaidia jeshi la Marekani kulitimuwa kundi hilo katika jimbo hilo.
Hatua yao hiyo ilikuja kujulikana kama Mwamko wa Anbar.
Takriban wanajeshi 25,000 wa Marekani walikuwa wamewekwa katika jimbo la Anbar.Kufuatia kukabidhiwa kwa jimbo hilo kwa Wairaq vikosi vya Marekani vitawekwa kwenye kambi zao nje ya miji na vitakuwa tu vinaonekana wakati vitakapoombwa.
Iraq na Marekani zinasema ziko karibu kufikia makubaliano juu ya mkataba mpya wa usalama ambao utaviongoza vikosi vya Marekani nchini Iraq baada ya kumalizika kwa mamlaka ya Umoja wa Mataifa mwishoni mwa mwaka.