1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yakanusha kutaka kuondoa wanakeshi wake Iraq

Yusra Buwayhid
7 Januari 2020

Licha ya mivutano kuzidi kuongezeka Iraq kufuatia mauaji yaliyofanywa na Marekani ya Jenerali wa Iran, Marekani imekanusha kuondoa majeshi yake nchini humo. Ujerumani hata hivyo itapunguza idadi ya wanjeshi wake.

Symbolbild: USA ziehen Truppen aus dem Irak ab
Picha: picture-alliance/dpa/K. Talbot

 Mnamo Januari 2, Rais wa Marekani Donald Trump aliamrisha shambulizi dhidi ya Jenerali wa ngazi ya juu Qassem Soleimani wa kikosi cha Qudus cha jeshi la Ulinzi wa Mapinduzi la Iran, kufuatia kifo cha kontrakta wa Marekani nchini Iraq. Na sasa raia wa Iran wakiwa wanaaomboleza kifo cha jenerali huyo, maafisa wa Marekani wanasema hatua zitakazochukuliwa na Iran ambayo ni adui wao wa muda mrefu, zitaamua hatma ya mgogoro huo uliozuka hivi karibuni. Afisa mmoja amesema, Marekani inategemea shambulizi kubwa kutoka Iran katika siku chache zijazo.

Soma zaidi: Mkanyagano mkubwa watokea wakati wa mazishi ya Soleimani

Jumatatu Waziri wa Ulinzi wa Marekani Mark Esper alikanusha kuwa majeshi yake yanapanga kuondoka nchini Iraq. Esper aliyasema hayo baada ya barua kusambaa inayopendekeza Marekani itaondoa majeshi yake kufuatia kura iliyopigwa na wabunge wa Iraq mwisho wa juma lililopita inayowataka kufanya hivyo.

"Nadhani watu wa Iraq hawataki tuondoke. Wanajua kuwa Marekani iko huko kuwasaidia kuwa nchi huru, na yenye maendeleo. Hiyo sio nia ya Iran. Iran inataka kuwadhibiti kama jimbo, na nadhani kuna wabunge wengi wa Iraq wanaoamini hivyo, alisema Mark Esper akiwa mbele ya waandishi habari.

Wanajeshi wa Marekani wakielekea Iraq - Januari 1, 2020Picha: picture-alliance/R. Haake

Marekani yaikosoa Urusi na China

Aidha Marekani pia imeikosoa Urusi na China, kwa kulizuia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa tamko la kukemea maandamano ya vurugu yaliyofanywa mjini Baghdad wiki iliyopita.

Mabalozi wa Urusu na China wamesema hawaungi mkono shambulizi hilo, lakini walipinga kutolewa taarifa rasmi kwa sababu haikutaja mauaji ya Jenerali wa Iran Qassem Soleimani yaliyofanywa na Marekani. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa haliwezi kutoa tamko lolote bila ya kuridhiwa na nchi wanachama wote 15.

Ujerumani kwa upande wake imesema baadhi ya wanajeshi wake waliotumwa Iraq watapelekwa nchini Jordan na Kuwait, kutokana na mivutano iliyoongezeka kufuatia mauaji ya jenerali Soleimani.

Kambi za kijeshi za Ujerumani hasa katika mji mkuu wa Baghdad na wa Taji zitapunguzwa idadi ya wanajeshi "kwa muda,"  Waziri wa Ulinzi Annegret Kramp-Karrenbauer na Waziri wa Mambo ya Nje Heiko Maas wameandika katika barua iliyotumwa kwa wabunge wa Ujerumani na nakala yake kuonekana na shirika la habari la dpa Jumanne.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW