1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Marekani yakataa kuipa ndege za kisasa Ukraine

31 Januari 2023

Rais wa Marekani Joe Biden amesema nchi yake haitapeleka nchini Ukraine ndege zake za kisasa za kivita chapa ya F-16.

F-16 Kampfjet der U.S. Air Force
Picha: Sgt. Joseph Swafford/abaca/picture alliance

rais Biden amesema hayo wakati ambapo serikali mjini Kyiv ikitanua orodha ya silaha inazozitaka kuweza kuvifurusha vikosi vya Urusi kutoka maeneo yanayokaliwa. Wiki iliyopita mataifa ya Magharibi zikiwemo Marekani na Ujerumani yaliidhinisha upelekaji wa vifaru vizito vya kivita nchini Ukraine, lakini alipoulizwa na waandishi habari jana iwapo anaunga mkono kutuma ndege aina ya F-16 nchini Ukraine, Rais Biden alisema hapana. Nchini Ukraine kwenyewe, mapigano yanaripotiwa kuendelea kupamba moto katika maeneo muhimu ambako Urusi inataka kupanua udhibiti wake kwenye mkoa wa Donetsk, mashariki mwa Ukraine. Kiongozi wa mkoa huo aliyeteuliwa na Kremlin, Denis Pushilin, alidai vikosi vya Urusi vinasonga mbele karibu na mji wa kimkakati wa Vugledar, lakini Kyiv imekanusha madai hayo, huku ikikiri kuwa mapigano ni makali huko.