1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yakubali kuondolewa ulinzi wa hatimiliki ya chanjo

6 Mei 2021

Serikali ya Marekani imetangaza kuunga mkono miito ya kimataifa ya kuondoa ulinzi wa hatimiliki za utengenezaji wa chanjo za Covid-19, hatua ambayo inatoa matumaini kwa mataifa masikini.

USA | COVID-19-Impfprogramm | Joe Biden Rede
Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Serikali ya Marekani imetangaza kuunga mkono miito ya kimataifa ya kuondoa ulinzi wa hatimiliki za utengenezaji wa chanjo za Covid-19, hatua inayotoa matumaini kwa mataifa masikini yanayokabiliwa na changamoto za kupata chanjo hizo huku Umoja wa Ulaya nao ukiunga mkono hatua hiyo. 

Mwakilishi wa Biashara wa Marekani Katherine Tai amesema kuwa katika wakati ambapo hakimiliki za uvumbuzi zina umuhimu, lakini Marekani inaunga mkono kusitishwa kwa ulinzi huo kwa chanjo za Covid-19 ili kumaliza janga hilo. Amesema hili ni janga la afya la kiulimwengu, na kuongeza kuwa hali ambayo si ya kawaida iliyosababishwa na maradhi hayo pia inahitaji kukabiliwa kwa hatua ambazo si za kawaida.

Rais Joe Biden wa Marekani amekuwa akikabiliwa na shinikizo kubwa la kumtaka kuweka msamaha wa ulinzi wa hatimiliki kwa watengezaji wa chanjo, na hususan katika wakati ambapo kuna ukosoaji kwamba mataifa tajiri yalikuwa yakijilimbikizia chanjo.

Soma Zaidi: Guterres: Dunia yahitaji mkakati wa kilimwengu wa kutoa chanjo 

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya ulimwenguni WHO Tedros Adhanom Gebreyesus ameuita uamuzi huo wa Marekani kuwa wa kihistoria na unaoashiria hatua kubwa katika kukabiliana na janga la COVID-19.

Rais wa Halmashauri ya Ulya Ursula von der Leyen amesema Ulaya pia itaangazia pendekezo hilo la MarekaniPicha: Olivier Hoslet/AFP/Getty Images

Hatua hii ya Marekani pia inaungwa mkono na Umoja wa Ulaya baada ya mapema leo rais wa Halmashauri kuu ya umoja huo, Ursula von der Leyen kutangaza kwmaba umoja huo uko tayari kujadiliana pendekezo la Marekani la kuondoa ulinzi wa hatimiliki katika uzalishaji wa chanjo hizo, ili kuongeza uzalishaji wake na kuwezesha upatikanaji zaidi wa chanjo hizo kwa kila taifa.

"Umoja wa Ulaya pia uko tayari kujadiliana juu ya pendekezo la kuushughulikia mzozo uliopo kwa ufanisi na kwa nadharia ya vitendo. Na ndio maana tuko tayari kujadiliana namna ambavyo pendekezo la Marekani la kuondoa ulinzi wa hatimiliki kwa chanjo za COVID linavyoweza kusaidia kufikia lengo hilo." amesema Leyen.

Akiwa mjini Brussels, Von der Leyen pia ametangaza kwamba Umoja wa Ulaya unakaribia kusaini makubaliano ya kupata dozi zaidi ya bilioni 1.8 kutoka kwa kampuni ya Pfizer-BioNTech, kuanzia miezi michache ijayo hadi mwaka 2023.

Wakati haya yanaendelea India inazidi kuelemewa na maambukizi mapya ya virusi vya corona, wakati hii leo kwa mara nyingine ikirekodi idadi ya juu zaidi ya vifo kwa siku, huku wasiwasi ukizidi kuongezeka. Takwimu za serikali zinaonyesha rekodi ya vifo 3,980 katika kipindi cha masaa 24 na kufanya jumla ya vifo tangu kuanza kwa janga hilo kufikia 230,168.

Siku ya Jumamosi India iliweka historia ya kuwa taifa la kwanza kwa rekodi ya kila siku ya maambukizi iliyopindukia 400,000. Virusi vinavyojibadilisha vinaendelea kuliweka taifa hilo katika hali ngumu zaidi wakati likipambana na upungufu wa mitungi ya Oksijeni na vitanda mahospitalini.

Mshauri mkuu wa serikali wa masuala ya sayansi K Vijay Raghavan amesema pamoja na hali inayoshuhudiwa sasa, taifa hilo la watu bilioni 1.3 bado linatakiwa kujiandaa na wimbi jipya la maambukizi

 Mashirika: AFPE/RTRE