1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yakumbuka mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11

11 Septemba 2016

Marekani Jumapili (11.09. 2016) imekuwa na kumbukumbua ya miaka 15 ya mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea nchini humo mwaka 2001 ambapo Rais Barack Obama amesema tishio la ugaidi limekuwa.

Picha: picture-alliancedpa/J. Taggart

Marekani Jumapili (11.09. 2016) imekuwa na kumbukumbua ya miaka 15 ya mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea nchini humo mwaka 2001 ambapo Rais Barack Obama amesema tishio la ugaidi limekuwa.

Magaidi walifanya mashambulizi hayo ya kujitowa muhanga kwa kuziteka nyara ndege nne za abiria na kuzibamiza kwa majengo mawili ya vituo vya biashara mjini New York na jengo la wizara ya ulinzi nje ya mji wa Washington ambapo takriban watu 3,000 waliuwawa.

Akizungumza Jumapili katika wizara ya ulinzi ya Marekani Obama amesema " Miaka 15 ya mapambano hayo tishio hilo limekuwa"

Obama amesema aina ya ugaidi imebadilika kutoka mashambulizi yanayosababisha maafa ya watu wengi na kuwa mashambulizi yanayofanywa na mtu mmoja mmoja ambayo yanakuwa ya kiwango kidogo lakini bado ni ya maafa.Ametaja mashambulizi ya risasi yaliofanywa na Waislamu wa itikadi kali huko San Bernadino na Orlando kama mifano.

Kumbukumbu imefanyika kwa kubakia kimya kwa dakika moja kuanzia saa 8:46 wakati hasa ndege ya kwanza iliotekwa nyara ilipobamizwa na jego la kituo cha biashara la kaskazini mjini New York.Majina ya wahanga 2,977 yalisomwa hadharani wakati wa ibada kuu ya kumbukumbu iliofanyika katika Makumbusho ya Taifa ya Kumbukumbu ya Septemba 11 mjini New York.

Zaidi ya watu milioni 23 wamelitembelea eneo hilo la kumbukumbu tokea lilipofunguliwa hapo Septemba mwaka 2011 na zaidi ya watu milioni 4 wameizuru makumbusho hiyo iliofunguliwa hapo mwezi wa Mei mwaka 2014.

Mashambulizi mabaya kabisa kufanyika Marekani

Ibada za kumbukumbu pia zimefanyika Washington na katika eneo la kumbukumbu la Shanksville nje kidogo ya Pennsylavania ambapo ndege ya nne ilianguka baada ya abiria wake inavyoonekana walipambana na wateka nyara na kusababisha ndege hiyo kuangukia shambani na kuepusha shambulio dhidi ya mji wa Washington.

Rais Barack Obama akizungumza wizara ya ulinzi.Picha: Reuters/J. Roberts

Mashambulizi hayo ya kigaidi ya Septemba 11 mwaka 2001 ni mabaya kabisa yaliosababisha maafa makubwa kuwahi kutokea katika ardhi ya Marekani na yamekuwa na taathira kubwa kwa sera ya ndani na ya nje ya nchi ya Marekani.

Hofu ya ugaidi imeendelea kuonekana dhahir na suala hilo pia limejitokeza sana katika kampeni za uchaguzi wa rais za mwaka huu wa 2016 ambazo ni za ushindani mkali kuwahi kushuhudiwa nchini humo.

Wananchi wasikubali kugawanya

Wapiga kura wamegawika sana juu ya njia bora ya kukabiliana na tishio la itikadi kali za Kiislamu ambapo mgombea wa chama cha Republikan Donald Trump ameshutumiwa kwa wito wake wa kutaka Waislamu wapigwe marufuku kuigia Marekani.Lakini Obama amesisitiza uwepo wa makabila tafauti nchini Marekani sio udhaifu bado ni na utaendelea kuwa mojawapo ya nguvu zake kuu. Amewataka wananchi wasikubali kuwaachia watu wawagawe.

Waombolezaji mjini New York.Picha: picture-alliance/newscom/J. Angelillo

Hofu ya wananchi wa Marekani ya kufanyika mashambulizi ya kigaidi imefikia kipeo cha juu hapo mwaka 2016 kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni wa Kituo cha Utafiti cha Pew wa hivi karibuni.

Hivi sasa wananchi wa Marekani wanaamini uwezo wa magaidi kufanya shambulio la kigaidi dhidi ya Marekani ni mkubwa zaidi kuliko ilivyokuwa wakati wa mashambulizi ya mwaka 2001.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa

Mhariri : Yusra Buwayhid

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW