1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiMarekani

Marekani yakumbwa na dhoruba kali zaidi ya baridi

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
23 Desemba 2022

Dhoruba kali ya baridi inayotokea angalau mara moja baada ya kipindi cha miaka 30 imeikumba Marekani. Hali hiyo imesababisha vurumai wakati watu wakijaribu kusafiri kwa ajli ya sikukuu ya Krisimasi.

Weltspiegel 02.02.2021 | USA New York City | Schneesturm
Picha: Brendan McDermid/REUTERS

Baridi hiyo kali iliyofikia nyuzi baridi chini ya sufuri imesababisha kuvunjwa kwa maalfu ya safari za ndege na kufungwa kwa viwanja vya ndege nchini Marekani.

Idara ya hali ya hewa nchini humo imetahadhrisha juu ya hali mbaya sana ya hewa kwenye majimbo kadhaa ya nchi hiyo. Idara hiyo imesema baridi inaweza kufikia chini ya nyuzi baridi 56 chini ya sufuri kipimo cha Celsius. Pana wasi wasi mkubwa wa kuharibika miundombinu na kusababisha vifo.

Theluji nyingi na upepo mkali umewafanya watu waahirishe mipango ya likizo.Tahadhari juu ya dhoruba ya baridi zimetolewa kwa mamilioni ya watu. Watabiri wa hali ya hewa wamesema baridi ni kali kiasi kwamba sehemu za mwili zinaweza kuganda katika muda wa dakika chache ikiwa mtu anatoka nje ya nyumba yake. Rais Joe Biden amesema baridi hiyo si ya mchezo.

Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Chip Somodevilla/Getty Images

Hali ya hatari kwenye barabara inazidi kuenea wakati ambapo wamarekani zaidi ya milioni 100 walikuwa  wanatarajiwa kwenda kwenye shughuli zao za kila siku. Baadhi ya barabara kubwa hazipitiki kabisa kaskazini mwa Marekani. Hata hivyo idara husika zinafanya bidii ya kurejesha hali kuwa ya kawaida.

Theluji nzito imeanguka na kufunika barabara. Safari za ndege 22,000 zilicheleweshwa na 1000 kati ya hizo zilivunjwa kabisa nyingi kati ya hizo kwenye viwanja vya ndege vya jimbo la Chicago. Baadhi ya watu waliamua kuendesha magari yao mwendo wa kilometa 1100. Gavana wa New York ameungana na magavana wa majimbo mengine kutangaza hali ya dharura na  ametahadharisha juu ya hatari ya kutokea maafa. Taarifa iliyotolewa imetahadharisha juu ya uwezekano mkubwa wa kutukia mafuriko, mgando wa barafu na  kukatika huduma za nishati.

Vyanzo:AFP/AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW