Marekani yalaani 'hofu', wakati wa kura ya maoni ya Burundi
22 Mei 2018Marekani imelaani kile ilichokitaja kuwa ni mazingira ya hofu, unyanyasaji na kutokuwepo uwazi katika kura ya maoni nchini Burundi ya marekebisho ya katiba ili kurefusha muhula wa kuhudumu kwa rais.
Siku ya Jumatatu, tume ya uchaguzi nchini Burundi ilitangza matokeo ya kura hiyo iliyofanyika Alhamisi wiki iliyopita ambapo kundi la ndio lililoongozwa na Rais Pierre Nkurunziza lilishinda kura hiyo kwa zaidi ya asilimia 73.
Ikiyatilia shaka matokeo hayo, wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema kura hiyo ya maoni ya tarehe 17 Mei ilikumbwa na ukosefu wa uwazi, vyombo vya habari kupigwa marufuku na majaribio ya kuwashinikiza na kuwatisha wapiga kura.
Nkurunziza mwenye umri wa miaka 54 ambaye amekuwa madarakani tangu 2005, sasa ana nafasi ya kusalia madarakani hadi mwaka 2034 baada ya kura hiyo ya maoni inayorefusha muhula wa kuhudumu kwa rais.
Taifa hilo la Afrika Mashariki limekumbwa na mzozo wa kisiasa tangu mwaka 2015 kufuatia Nkurunziza kugombea muhula wa tatu madarakani kinyume na sheria.