1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yalaani mauaji ya wapinzani nchini Msumbuji

22 Oktoba 2024

Marekani imelaani mauaji ya washirika wawili wa mgombea mkuu wa upinzani Msumbiji Venancio Mondlane, waliouawa kwa kupigwa risasi mwishoni mwa juma walipokuwa wakijiandaa kupinga uchaguzi uliofanyika mapema mwezi huu.

Msumbiji | Tukio la mkesha kufuatia mauaji ya Elvino Dias na Paulo Guambe
Wakili Elvino Dias wa mgombea mkuu wa upinzani nchini Msumbiji Venancio Mondlane, ambaye aligombea urais katika uchaguzi wa Oktoba 9, aliuawa kwa kupigwa risasi mjini Maputo Oktoba 19.Picha: ALFREDO ZUNIGA/AFP

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Matthew Miller ilisema kuwa inalaani mauaji ya wakili Elvino Dias na mgombea ubunge wa Podemos Paulo Guambe na kuongeza kuwa inaungana na wito uliotolewa na vyama vyote vya upinzani nchini Msumbiji kuhimiza uchunguzi wa kina wa uhalifu huo. Wawili hao waliuawa wakati gari lao lilipozingirwa na magari mengine katika mji mkuu Maputo kabla ya uchaguzi uliofanyika oktoba 9.Msumbijiimeshuhudia machafuko baada ya ya zoezi la upigaji kura, huku polisi wa kutuliza ghasia wakiwatawanya umati wa watu mjini Maputo hapo jana wakipinga madai ya udanganyifu katika uchaguzi. Rais Filipe Nyusi baada ya mihula yake miwili anaachia ngazi lakini mgombea wa chama chake cha FRELIMO, Daniel Chapo, anatarajiwa kushinda katika matokeo ya uchaguzi ambayo yatatangazwa wiki hii.