Marekani yalaani utekaji madaraka Bangui
27 Machi 2013"Tunalaani kwa nguvu zote hatua ya waasi wa muungano wa Seleka kumfukuza rais Francois Bozize, Michael Djotodia kujitangaza kuwa rais na tangazo la kusitisha katiba na bunge la Jamhuri ya Afrika ya Kati'', amesema Patrick Ventrell, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani. Ventrell amesema uongozi wa Seleka sharti ubebeshwe dhamana kwa uharibifu uliosababishwa na mapigano na uporaji wa miezi kadhaa.
Mawakili wa wizara hiyo wanatathmini kama utekaji huo wa madaraka unaendana na maana ya mapinduzi, hatua ambayo itasaidia kupitisha uamuzi kuhusu msaada wa Marekani kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Ventrell amesema wanataka waasi wa Seleka waondoke madarakani na wamuachie waziri mkuu Nicolas Tiangaye na serikali yake aiongoze nchi.
Uporaji mali walaaniwa
Wakati huo huo, makundi ya utoaji misaada na jamii ya kimataifa jana zilikosoa uporaji uliotapakaa kila mahali katika mji wa Bangui. Shirika la Madaktari wasio na mipaka, Medicins Sans Frontieres, limesema machafuko yanayoendelea Jamhuri ya Afrika ya Kati yanawazuia wagonjwa waliojeruhiwa vibaya kupata msaada wanaouhitaji.
Marie-Servane Desjonquéres, afisa anayeshughulikia masuala ya Jamhuri ya Afrika ya Kati katika Shirika la Msalaba mwekundu mjini Geneva, Uswisi, anasema, "Bado ni shida kuzungumzia kwa uhakika kuhusu hali wanayokumbana nayo watu mjini Bangui. Bado hakuna huduma za umeme; jambo linaloweza kusababisha matatizo ya jinsi ya kuendesha shughuli za baadhi ya miundombinu kwa mfano vituo vya afya." Bi Desjonquéres aidha amesema kuna watu waliojeruhiwa na shirika la msalaba mwekundu limekusanya maiti."
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Martin Nesirky, pia amesema jana kwamba wizi wa mali unaendelea katika sehemu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na hospitali moja ya watoto. Viongozi wa waasi wamekuwa wakiwasaka waporaji wanaotembea katika barabara za mji wa Bangui.
Zaidi ya waasi 1,000 wa muungano wa Seleka waliushambulia mji mkuu Bangui Jumamosi iliyopita, na kumlazimu rais Francois Bozize kukimbilia uhamishoni nchini Cameroon. Mapigano makali yalisababisha vifo vya wanajeshi wasiopungua 13 wa Afrika Kusini na idadi isiyojulikana ya raia.
Mwito wa kufanya uchunguzi Afrika Kusini
Serikali ya Afrika Kusini inakabiliwa na miito ya kufanya uchunguzi kwa nini wanajeshi wake walipelekwa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Mauaji ya wanajeshi 13, yanaelezwa kuwa mabaya kabisa kulikabili jeshi la Afrika Kusini tangu kumalizika utawala wa ubaguzi wa rangi. Yamezua maswali kwa nini jeshi la Afrika Kusini lilikuwa mjini Bangui, sababu rasmi ikiwa ni kutoa mafunzo kwa majeshi ya nchi hiyo.
Chama kikuu cha upinzani cha Afrika Kusini, Democratic Alliance, kimesema kutumwa kwa wanajeshi hao kunakotiliwa shaka, sharti kufanyiwe uchunguzi wa kina na bunge. Waziri kivuli wa chama kikuu cha upinzani, Democratic Alliance, David Maynier, amesema ukweli ni kuwa hawafahamu kwa nini wanajeshi walipelekwa Bangui na ndio maana wanataka uchungzi wa kina ufanywe na bunge. Ameongeza kusema kuna tetesi wanajeshi hao walipelekwa kumsaidia rais Bozize.
Mwezi Januari mwaka huu rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, aliamuru kutumwa wanajeshi Jamhuri ya Afrika ya Kati kama sehemu ya mkataba wa ushirikiano. Wanajeshi 400 waliidhinishwa, lakini 200 pekee ndio waliokwenda. Waziri Maynier amesema uchunguzi unatakiwa kulenga kubaini kama rais Zuma aliwaelekeza vibaya wabunge kuhusu sababu za kuwatuma wanajeshi hao.
Mwandishi: Josephat Charo/APE/DPAE/AFPE
Mhariri: Daniel Gakuba