1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yalaumiwa kujiondoa Baraza la Haki za Binaadamu

20 Juni 2018

Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa lilirejea kwenye shughuli zake za kawaida leo, licha ya Marekani kutangaza kujiondowa, hatua iliyozusha shutuma dhidi ya taifa hilo lenye nguvu kubwa duniani.

UN-Hochkommissar Menschenrechte Said Raad al-Hussein
Picha: picture-alliance/Keystone/M. Trezzini

Kikao cha Jumatano (Juni 20) cha Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva kilichozungumzia mauaji ya makusudi na uhuru wa kujieleza, kilifanyika huku kiti cha Marekani kikiwa kitupu, baada ya Balozi wake, Nikki Haley, kutangaza kuiondoa nchi yake huku akilikosoa vikali baraza hilo kwa kile alichosema ni "chuki za kupindukia dhidi ya Israel" na akilioteza kidole kwa kuwa kwake na wajumbe ambao wenyewe ni wavunjaji wakubwa wa haki za binaadamu, kwa kuzitaja China, Cuba, Venezuela na Congo.

Umoja wa Ulaya ulikiita kitendo cha Marekani kujiondoa kwenye Baraza hilo kuwa ni cha kusikitisha. Balozi wa Bulgaria kwenye Baraza hilo ambaye alizungumza kwa niaba ya Umoja wa Ulaya, Deyana Kostadinova, aliufananisha uamuzi huo na hujuma dhidi ya Marekani yenyewe.

"Umoja wa Ulaya unasikitishwa na uamuzi huu wa Marekani kujiondoa kwenye Baraza la Haki za Binaadamu. Kwa miaka mingi, Marekani imekuwa mshirika madhubuti wa Umoja wa Ulaya kwenye Baraza hili. Uamuzi huu wa jana unatishia kulihujumu jukumu la Marekani kama mtetezi madhubuti na muungaji mkono wa demokrasia duniani," Kostadinova aliliambia Baraza hilo mjini Geneva siku ya Jumatano (Juni 20).

Urusi yaikosoa Marekani

Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, ameiondoa nchi yake kwenye Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja huo.Picha: Reuters/T.S. Jordan

Muda mchache baadaye, Urusi, hasimu mkubwa wa Marekani, likawa miongoni mwa mataifa ya mwanzo mwanzo kuzungumzia hatua hiyo iliyowashituwa wengi, ikisema kuwa Marekani ilichukuwa hatua ya "kitoto na inayovunja heshima yake kwenye masuala ya haki za binaadamu."

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi, Maria Zakharova, alisema Marekani imeshindwa hata kuangalia matatizo yake yenyewe ya haki za binaadamu, huku ikijidai kulifundisha kazi baraza hilo kwa maslahi yake ya kisiasa.

Kauli kama hiyo ilitolewa pia na serikali ya Palestina, ambayo ilisema: "Kujiondowa kwa Marekani kwenye Baraza la Haki za Binaadamu kunaonesha umbali ambao utawala huu uko tayari kwenda katika kuikingia kifua Israel isiwajibishwe."

Hanan Ashrawi, mwanachama wa ngazi za juu wa Chama cha Ukombozi wa Palestina, PLO, aliilaani kauli ya Haley, akisema ni ya "upotoshaji na uongo ulio wazi."

Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, aliita hatua hiyo kuwa ni uthibitisho wa hali ya juu wa kusema kuwa sasa imetosha. 

Hatua hii ya Marekani ni sehemu ya mkururo wa maamuzi ya utawala wa Trump yanayokosolewa vikali duniani.  

Tayari Trump ameshaiondowa Marekani kutoka makubaliano ya nyuklia ya Iran na pia mkataba wa mabadiliko ya tabia nchi wa Paris. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP/AP
Mhariri: Saumu Yussuf