1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yalipa kisasi dhidi ya magaidi Somalia

Angela Mdungu
3 Januari 2020

Marekani kulipa kisasi kwa magaidi walioshambulia Mogadishu, na uamuzi ya mahakama ya Angola juu ya kushikilia mali na akaunti za benki za Isabel dos Santos ni miongoni mwa mada zilizoandikwa na magazeti ya Ujerumani

Angola l Isabel dos Santos - Gericht zieht Vermögen
Picha: picture alliance/dpa/TASS/M. Metzel

Wiki hii, "Süddeutsche Zeitung" liliandika juu ya hatua zilizochukuliwa na Marekani baada ya shambulio la kigaidi lililofanywa mjini Mogadishu huko Somalia. Jeshi la Marekani limetumia ndege zisizo na rubani katika mashambulizi ya anga dhidi ya wapiganaji wa kundi la Al shabaab nchini Somalia.

Kituo cha oparesheni ya jeshi la Marekani barani Afrika AFRICOM kilithibitisha siku ya Jumapili kuwa mashambulizi ya kulipa kisasi baada ya tukio la Mogadishu yalikuwa yameratibiwa kwa kushirikiana na serikali ya Somalia. Jumla ya magaidi wane waliuawa katika mashambulizi matatu ya anga.

Gazeti hilo liliongeza kuwa taarifa za kiitelijensia zinasema mmoja wa waliouawa katika mashambulizi hayo ya anga ya kulipa kisasi ni afisa wa juu wa wanamgambo wa Al Shabaab. Katika shambulio la Jumamosi mjini Mogadishu, takriban watu 100 waliuawa.

Mwanamke tajiri zaidi Afrika matatani

Kwa upande wake gazeti la "Frankfuter Allgemeine", limeandika juu ya uamuzi wa mahakama nchini Angola kushikilia mali na akaunti za benki za Isabel dos Santos, mwanamke anayeaminika kuwa tajiri zaidi barani Afrika. Hatua hiyo ni kutokana na tuhuma za rushwa zinazomkabili Isabel ambaye ni mtoto wa rais wa zamani wa Angola Jose Eduardo dos Santos. Uamuzi huo ulitangazwa na mwanasheria mkuu wa serikali ya nchi hiyo mjini Luanda.

Serikali ya Angola inamtaka Isabel dos Santos kulipa dola bilioni moja za Kimarekani ikidai kwamba alizipata kwa njia zisizo halali. Hata hivyo mwanamama huyo amesema kuwa hana hatia na kwamba ataendelea kukipigania kile anachokiamini nchini humo. Kupitia ukurasa wake wa twitter aliandika kuwa ukweli utafahamika.

Gazeti hilo linaongeza kuwa, hilo wanatumaini pia raia milioni 30 wa Angola, nchi ya kusini mwa Afrika yenye utajiri wa mafuta na almasi ambapo wengi wao wanaishi kwa kutumia chini ya dola mbili kwa siku huku kundi la wanasiasa wasomi, wajasiriamali na majenerali wakimiliki mamilioni.

Mafanikio ya Maandamano Sudan na changamoto lukuki

"Die tageszeitung" lilianza kichwa cha habari kinachosema Wanawake wa Sudan wanaweza kujivunia. Gazeti hilo linasema raia wa Sudan wanafurahi kuwa maandamano yao makubwa yaliyoanza mwaka mmoja uliopita yamekuwa na mafanikio kwa kiasi Fulani lakini bado wanapambana na mgogoro mkubwa wa kiuchumi.

Maandamano ya raia wa nchi hiyo yalisababisha kung'olewa kwa rais Omar al-Bashir mnamo mwezi April baada ya kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji. Waziri mkuu Abdalla Hamdok ambaye ameongoza serikali ya Sudan tangu mwezi Agosti hapaswi kuonewa wivu kwa kazi yake, kwani si tu kuwa mchumi huyo anatakiwa kufanya kazi kwa tahadhari katika hali tete ya kisiasa, bali pia anahitaji kuunyanyua uchumi na kutatua migogoro ya silaha.

Asili ya Kobe wakubwa toka Mauritius

Nalo gazeti la "Der Tagesspiegel", liliandika juu ya asili ya kobe wakubwa wa Mauritius wanaosafiri umbali mrefu toka sehemu moja kwenda nyingine. Gazeti hilo lilianza kwa kuandika, Desemba 14, mwaka 2004, Kobe mkubwa aina ya Aldabra aliwasili katika pwani ya Tanzania. Ni aina ya kobe ambao huishi katika visiwa vya Shelisheli pekee umbali wa kilometa 2000 katikati mwa bahari ya hindi. 

Mwandishi wa habari hiyo aligusia pia juu ya viumbe hao adimu na kusema uwezo mkubwa wa kobe kuendelea kuishi kwa muda mrefu bila za kula na kunywa huenda  ndizo sababu hasa ni kwa nini wanyama hao na baadhi ya mamalia huishi katika visiwa vilivyo mbali.  Kobe hao wakubwa ambao waliishi katika visiwa vya Reunion, Mauritius na Rodrigues kwa miaka 200 iliyopita pia wanatokea mbali. Kwa mujibu wa  sehemu ya utafiti wa Christian Kehlmeier anasema baadhi ya kobe hao wakubwa wanatokea katika bara la Afrika.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW