Marekani yamtaka Waziri Mkuu wa Haiti kuandaa uchaguzi huru
7 Machi 2024Marekani imemtolea wito Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry kuharakisha upatikanaji wa kipindi cha mpito, wakati magenge ya wahalifu wenye silaha yakimtaka aondoke madarakani kufuatia kuyumba kwa usalama na uwepo wa mgogoro wa kibinaadamu katika taifa hilo la Karibiani.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Karine Jean-Pierre, amesema nchi hiyo inatoa wito kwa Henry kuandaa uchaguzi huru, ambayo ni mojawapo ya matakwa ya kiongozi wa magenge hayo yaliyo na nguvu. Jimmy Cherizier.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana kwa dharura kujadili hali ya kisiasa Haiti, limesema lina wasiwasi wa jinsi hali inavyozidi kuwa mbaya na kwamba kikosi cha kulinda amani kinapaswa kupelekwa huko mara moja.
Cherizier ameonya ghasia zinazoendelea huenda zikasababisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe iwapo Henry hatojiuzulu.