Marekani yamuonya Kabila kutogombea uchaguzi wa Desemba
27 Julai 2018Kauli kama hiyo imetolewa pia na wajumbe wengine wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, zikiwemo Uingereza na Ufaransa. Naibu Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Jonathan Cohen, amelieleza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba nchi yake inasikitika Rais Kabila hakuitumia hotuba yake ya Juali 19 wakati akilihutubia bunge "kuondoa utata uliopo kuhusu malengo yake".
"Tumebaki na miezi mitano kabla ya uchaguzi kufanyika", alisema Cohen akiongeza kwamba "muda wa kusuasua umekwisha". Taifa hilo kubwa na lenye utajiri wa madini liko chini ya shinikizo kuhakikisha linafanya uchaguzi huru Desemba 23, huku kukiwa na wasiwasi kwamba Kabila, ambaye amekuwepo madarakani tangu mwaka 2001, anaweza kujaribu kugombea tena au kung'ang'ania madaraka.
Kumalizika kwa Muhula wa Kabila
Muhula wa pili wa Kabila ulimalizika mwishoni mwa 2016 lakini alisalia madarakani kwa sababu ya kuchelewesha uchaguzi, hatua ambayo ilisababisha maandamano makubwa. Balozi wa Kongo kwenye Umoja wa Mataifa, Ignace Gata Mavita, hakutoa maelezo yoyote kuhusu nia ya Kabila, akidokeza tu kwamba zoezi la usajili wa wagombea urais lilifunguliwa siku ya Jumatano na litadumu hadi Agosti 8.
Hata hivyo, amedai kwamba jumuiya ya kimataifa inaingilia mchakato wa uchaguzi bila ya kutoa ufafanuzi zaidi. Gata amesema wakati sasa maandalizi ya uchaguzi yamewiva, serikali inatarajia vyama vyote vya Kongo pamoja na "washirika wake wa kimataifa ambao mara nyingi hufanya mipango ya kuingilia uchaguzi", waunge mkono zoezi la uchaguzi "kwa ufanisi kupitia matendo chanya".
Kwa upande mwingine, balozi huyo wa Kongo kwenye Umoja wa Mataifa amesema serikali ya nchi yake "inathamini uungwaji mkono wa washirika wa kikanda kama vile SADC", ambako Kongo ni mwanachama.
Maandalizi ya uchaguzi
Leila Zerrougui, mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Kongo, ameliambia Baraza la Usalama kupitia vidio kwamba uchaguzi "unazidi kuleta matarajio kwa Wakongo na jumuiya za kimataifa" na kwamba utaongeza usalama ndani ya Kongo na ukanda mzima.
"Ingawa maendeleo makubwa yamepatikana katika kukamilisha hatua muhimu katika ratiba ya uchaguzi, mchakato wa uchaguzi unabaki kuwa chanzo cha wasiwasi na kutoaminiana baina ya chama tawala na upinzani na kati ya upinzani na tume ya uchaguzi', alisema mjumbe huyo, akiongeza kuwa malalamiko ya upinzani yanajumuisha uamuzi wa serikali wa kutumia mashine za kielekroniki za kupigia kura, usajili wa uchaguzi na tume ya uchaguzi.
Cohen, naibu balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, ameitaka tume ya uchaguzi kutotumia mashine hizo za kielektroniki ambazo hazikujaribiwa na kutumia karatasi za kupigia kura ambazo 'zinaaminika".
Hata hivyo, Balozi wa Kongo kwenye Umoja wa Mataifa aliitetea tume ya uchaguzi ya nchi yake, CENI, akisema ilifanya "kampeni ya uelimishaji" juu ya masuala ya kiufundi na kiutendaji yanayojenga uaminifu na kutoa shaka kuhusiana na uchaguzi, na hususan mashine hizo za kupigira kura.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP
Mhariri: Mohammed Khelef