1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaongeza harakati za kupambana na Al Qaeda, Yemen.

Halima Nyanza28 Desemba 2009

Marekani kwa usiri imefungua safu ya tatu ya mapambano dhidi ya mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda nchini Yemen, huku wakati huohuo Rais Barack Obama akitaka nchi yake kutathmini upya usalama wake wa safari za anga.

Vikosi vya jeshi la Yemen, ambavyo vinapewa nguvu na Marekani katika operesheni kabambe ya kupambana na mtandao wa Al Qaeda nchini humo.Picha: AP

Likimnukuu afisa wa zamani wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA, ambaye hakutajwa jina, gazeti la New York Times la Marekani limesema mwaka mmoja uliopita CIA, ilituma wafanyakazi wake waliobobea katika masuala ya kupambana na ugaidi nchini Yemen, na wakati huohuo baadhi yao kuanza kutoa mafunzo kwa jeshi la Yemen juu ya mbinu za kupambana na ugaidi.

Wizara ya Ulinzi ya Marekani itatumia zaidi ya dola milioni 70 katika kipindi cha miezi 18 ijayo kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa kikosi maalumu na kuliandaa jeshi la Yemen.

Msaada huo wa fedha pia utaigusa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Yemen.

Marekani imekuwa ikiilenga zaidi Yemen baada ya raia wa Nigeria ambaye alijaribu kuilipua ndege ya nchi hiyo, wakati ilipokuwa ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Detroit wakati wa sikukuu ya Krismasi, kukiri kupata mafunzo ya kutengeneza mabomu yaliyotolewa na Al Qaeda nchini Yemen.

Kwa upande mwingine, Yemen imeelezwa kwamba ni kimbilio la watu wenye misimamo mikali ya kidini, kutokana na kwamba serikali ya nchi hiyo iliwakaribisha wapiganaji wa kiislamu ambao walikuwa wakipigana nchini Afghanistan miaka ya 80.

Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, katika miaka ya hivi karibuni wapiganaji wa Al Qaeda juhudi zao zimelenga kujenga ngome nchini Yemen, kuandikisha wapiganaji kutoka maeneo mbalimbali ya kanda hiyo, kushambulia balozi za kigeni na vitega uchumi vingine.

Wakati huohuo, Rais Barack Obama wa Marekani ametaka kupitiwa upya kwa orodha ya watu ambao hawatakiwi kusafiri kuelekea nchini humo baada kutokea kwa jaribio hilo la kigaidi la kulipua ndege lililotokea siku ya Krisma na kutaka pia kujua mtu aliyehusika na jaribio hilo aliwezaje kuingia katika ndege hiyo na vifaa vya milipuko alivyotumia kufanya jaribio hilo.

Hata hivyo kwa upande wake akimzungumzia mtuhumiwa huyo, raia wa Nigeria huyo Umar Farouk Abdulmutallab Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani Janet Napolitano amesema hakuna ishara kwamba mnigeria huyo alikuwa ni sehemu ya mpango wa njama kubwa na kuonya kuhusiana na uvumi kwamba amepewa mafunzo na Al Qaeda.

Mtuhumiwa huyo kwa sasa anashikiliwa katika gereza moja lililoko Detroit, Marekani.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri:

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW