1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Marekani yaongeza msaada kwa Sudan kupambana na njaa

15 Juni 2024

Marekani imetangaza msaada mwingine wa dola milioni 315 kwa ajili ya kuwasaidia raia wa Sudan wanaokabiliwa na njaa kutokana na vita vya wenyewe wa wenyewe vilivyopindukia mwaka mmoja.

Mkimbizi wa Sudan
Vita nchini Sudan vimewalazimisha mamilioni ya watu kuwa wakimbizi. Picha: Albert Gonzalez Faran/Unamid/Han/dpa/picture alliance

Msaada huo utajumuisha chakula na maji ya kunywa pamoja na kutoa huduma za matibabu ikiwemo uchunguzi na tiba kwa watoto walio na utapiamlo.

Umetolewa katika wakati makadirio yanaonesha kiasi watu milioni 5 ndani ya Sudan wanakabiliwa na njaa kali na chakula pia hakipatikani kwenye mataifa jirani ambako raia milioni 2 wa Sudan wamekimbilia kuepuka mapigano.

Tangazo la msaada huo wa Marekani limeambatana na wito wa serikali mjini Washington wa kuzirai pande hasimu kukomesha tabia ya kuzuia usambazaji wa mahitaji ya kiutu kwa raia.

Mashirika ya misaada ya kimataifa ikiwemo lile la Marekani, USAID yametoa hadhari kwamba Sudan inaelekea pabaya na ukosefu wa chakula unaweza kuzusha baa la njaa kushinda lile lililoikumba Ethiopia mwanzoni mwa miaka 1980.

Licha ya miito ya kimataifa pande hasimu ambazo ni jeshi la nchi hiyo na kikosi cha wanamgambo wa RSF bado wanapambana kuwania madaraka.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW