1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaisaidia Ukraine, Urusi ikidai ushindi Mariupol

22 Aprili 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ameishukuru Marekani kwa msaada mpya wa kijeshi wenye thamani ya dola milioni 800 akidai "hicho ndicho walichokuwa wakikisubiri."

USA Washington Weißes Haus | Ukraine-Statement Joe Biden, Präsident
Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Kiongozi huyo ameyataka mataifa ya Magharibi kuharakisha mchakato wa kuwasilisha misaada ya kijeshi nchini humo ili kuisaidia nchi yake kukabiliana vilivyo na mashambulizi ya Urusi.

Msaada huo wa kijeshi uliotangazwa Alhamis na Rais Joe Biden unajumuisha silaha nzito za kivita na ndege zisizo na rubani ili kusaidia katika mapambano yanayozidi katika eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine.

Wakati huo huo Rais Zelenskiy pia amewatahadharisha raia wa Ukraine wanaoishi kusini mwa nchi hiyo katika miji inayodhibitiwa na majeshi ya Urusi, dhidi ya kuwapa vitambulisho vyao akidai huenda wakavitumia "kufanya kura ya uongo ya maoni" ili wabuni serikali rafiki kwa Urusi.

Urusi kuiteka Mariupol utakuwa ushindi mkubwa

Huku hayo yakiarifiwa Rais Vladimir Putin amedai Urusi imeshinda vita vya mji wa Mariupol licha ya takriban wapiganaji elfu 2 wa Ukraine kudaiwa kwamba bado wamejificha katika kiwanda kimoja kikubwa cha chuma mjini humo. Putin ameviamrisha vikosi vya Urusi visifanye mashambulizi katika mji huo badala yake viufunge kabisa ili kusiwe na mwanya wa kuingia mtu yeyote.

Kiwanda cha chuma cha Azovstal waliko wanajeshi wa Ukraine MariupolPicha: Musienko Vladislav/Ukrainian News/IMAGO

Urusi inaonekana kuudhibiti mji huo wa kimkakati wa kusini sasa, ikiwemo bandari yake muhimu ambayo imeharibiwa vibaya mno baada ya karibu miezi miwili ya mashambulizi ya mabomu.

Inaripotiwa kwamba Urusi inataka kutumia mbinu ya kuizingira Mariupol na kuwasubiri wanajeshi wa Ukraine walioko katika kiwanda hicho cha chuma kujisalimisha mara watakapoishiwa na silaha au chakula.

Lakini Meya wa mji wa Mariupol Vadym Boychenko amekanusha vikali madai ya Putin kwamba mji huo umetekwa na Urusi.

Kuuteka mji wa Mariupol utakuwa ni ushindi mkubwa mno kwa Urusi katika vita dhidi ya Ukraine kwa kuwa itaweza kudhibiti sehemu kubwa zaidi ya pwani, itamaliza ujenzi wa daraja litakaloiunganisha Urusi na rasi ya Crimea ambayo iliiteka mwaka 2014 na hii itatoa nafasi ya majeshi zaidi kujiunga na mapambano yanayoendelea sasa eneo la mashariki katika kitovu cha viwanda cha Ukraine, mji wa Donbas.

Makaburi ya halaiki kama yaliyogunduliwa Bucha

Kwengineko naibu Waziri Mkuu wa Ukraine Iryna Vereshchuk katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram amesema, hakuna wakaazi wa Mariupol waliookolewa jana kutokana na mashambulizi ya mabomu ya Urusi katika njia zilizokubaliwa za kutoa misaada ya kiutu.

Wa-Ukraine waapa kutetea maeneo yao

02:15

This browser does not support the video element.

Naye Meya wa Mariupol Vadym Boychenko anasema huenda ikawa zaidi ya raia elfu 9 wamezikwa katika makaburi ya halaiki katika kijiji cha Manhush nje ya mji huo. Boychenko ametaka jamii ya kimataifa kulaani mauaji yanayoendelea kufanywa na Urusi.

Katika taarifa ya kando aliyoitoa mapema Alhamis, meya huyo alidai wanajeshi wa Urusi wamechimba mahandaki karibu na kijiji cha Manhush na wanaficha uhalifu wao wa kivita kwa kutupa miili ya watu huko. Amedai miili ya Waukraine waliouwawa ilianza kupotea mitaani na wanajeshi hao ndio waliokuwa wakiichukua na kwenda kuitupa.

Vyombo vya habari vya Ukraine vimechapisha picha za setlaiti za Manhush zinazoonyesha kile inachosema ni makaburi ya halaiki sawa na yale yaliyogunduliwa Bucha. Madai na picha hizo lakini havikuweza kuthibitishwa wakati huo wa uchapishaji.

Chanzo: AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW