1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaongoza COVID-19, China yatangaza ushindi

30 Machi 2020

Maambukizi ya kirusi cha corona yamepindukia 100,000 nchini Marekani na kulifanya taifa hilo kuongoza duniani, katika wakati ambapo China, ambayo ilianza kuwa na wagonjwa wa mwanzo ikitangaza kukidhibiti kirusi hicho.

Coronavirus - Südkorea
Picha: picture-alliance/dpa/AP/A. Young-Joon

China inasema kuna wagonjwa wapya 31 wa ugonjwa wa COVID-19 na vifo vinne hivi leo, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Kamisheni ya Afya ya nchi hiyo.

Miongoni mwa wagonjwa hao 31, thalathini walitoka nje ya nchi hiyo, na ni mmoja tu aliyeambukizwa katika jimbo la kaskazini magharibi la Gansu.

Wanne waliofariki dunia ni kwenye jimbo la Hubei, kiini cha maambukizi ya kirusi cha corona, ambalo hata hivyo halina mgonjwa mpya. Jimbo hilo lililokuwa kwenye marufuku ya kutotoka nje, limeanza kurejea kwenye maisha yake ya kawaida.

Maambukizi kutoka nje ndicho kikwazo kikubwa kwa China kwa sasa, baada ya hapo jana Baraza lake la Taifa kutangaza kwamba kimsingi nchi hiyo imefanikiwa kuuzuwia ugonjwa wa COVID-19.

Tangu kirusi hicho kianze kusambaa mwezi Disemba mwaka jana, watu 81,470 wameambukizwa nchini China pekee, ambako 3,304 wamepoteza maisha. 

Marekani yaongoza kwa maambukizi


Nchini Marekani, idadi ya walioambukizwa imefikia 142,000, huku waliopoteza maisha wakipindukia 2,500.

Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: picture-alliance/dpa/M. Dimestico

Katika jimbo la New York pekee, watu zaidi ya 1,000 wameripotiwa kufa, ikiwa ni chini ya mwezi mmoja tangu mgonjwa wa mwanzo kugundulika kwenye jimbo hilo.

Kufikia jioni ya jana, eneo la mjini la jimbo hilo lilitangaza kuwa vifo vimefikia 776, huku miji mingine ikitangaza vifo 250, na hivyo kuifanya idadi kamili ya waliopoteza maisha kwa ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na kirusi hicho kufikia 1,026.

Hayo yanakuja wakati Rais Donald Trump akitangaza kwamba huenda vifo vyote vitavyotokana na kirusi hicho vikapindukia 100,000 nchini Marekani. Trump ameongeza muda wa watu kujitenga ili kuepuka maambukizi mapya hadi tarehe 30 mwezi Aprili.

Muda wa awali uliowekwa ulikuwa wa wiki mbili, ambao unamalizika leo.

Meli yenye wagonjwa wa COVID-19 yazuiwa kutia nanga
 

Picha: Getty Images/P. Kane

Abiria kwenye meli ya kifahari yenye watu walioambukizwa kirusi cha corona na ambayo imekwama nchini Panama, wameambiwa kwamba bado kampuni inayomiliki meli hiyo inatafuta bandari itakayokubali kuwapokea, siku kadhaa baada ya kutuma maombi maalum ya msaada.

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Kampuni ya Holland America Line, Orlando Ashford, baada ya meya wa mji mmoja wa jimbo la Florida nchini Marekani kusema kuwa hawako tayari kuipokea meli hiyo.

Orlando amewaambia abiria hao kupitia ujumbe wa video kuwa bado wanajaribu kuangalia mahala pa kuwashusha, huku watu wanne ndani ya meli hiyo wakiwa wamefariki kutokana na ugonjwa COVID-19.

Meli hiyo ya kifahari iitwayo Zaandam imekwama kwenye Bahari ya Pasifiki tangu tarehe 14 mwezi huu wa Machi, baada ya baadhi ya watu miongoni mwa abiria wake 1,800 kuanza kuuguwa ugonjwa wa mafua, na bandari kadhaa za Amerika Kusini kuikatalia kutia nanga.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW