Marekani yaongoza medali olimpiki ya walemavu
18 Machi 2018Mji wa Pyeongchang ambao pia ulikuwa mwenyeji wa michuano ya mwezi uliopita ya olimpiki ya majira ya baridi, uliwakaribisha jumla ya wanariadha walemavu 567 katika michuano hiyo ili kushindania medali 80.
Marekani imeondoka na medali 13 za dhahabu, 15 za fedha na 8 za shaba. Wanariadha walemavu wa Urusi ambao walibainika kutotumia dawa za kuongeza nguvu mwilini, waliruhusiwa kushiriki michuano hiyo na kumaliza katika nafasi ya pili na Canada imeshika nafasi ya tatu.
Kama ilivyo kwa michezo ya Olimpiki, timu ya Urusi kwa ujumla wake ilipgwa marufuku kushiriki michezo hiyo kutokana na kubainika kutumia pakubwa dawa za kuongeza nguvu.
Mslovakia, Mfaransa wang'aa
Washiriki bora mmoja mmoja katika michezo hiyo ya olimpiki ya walemavu ya majira ya baridi walikuwa Hnerieta Farkasova kutoka Slovakia, na Marie Bochet wa Ufaransa wenye medali nne za dhahabu katika michezo ya kuteleza kwenye barafu.
Michezo hii ya olimpiki ya walemavu ndiyo ilikuwa ya kwanza kuwashirikisha wanariadha wa Korea Kaskazini, katika ishara nyingine ya kujongeleana kati ya Korea mbili kufuatia maendeleo makubwa yaliofikiwa wakati wa olimpiki.
Ingawa ujumbe wa Korea Kaskazini ulikuwa tayari umeondoka, bendera yao ilibebwa katika hafla ya ufungaji na mtu kujitolea kabla ya kuzimwa kwa mwenge wa michezo hiyo kuzimwa.
""Hata kama mwenge ukizimwa, utawaleta watu wa mataifa hayo mawili pamoja," alisema Lee Beom, kiongozi wa kamati ya maandalizi.
Chini ya moto ya "tunasogeza ulimwengu", sherehe ya kufunga ilipambwa kwa maonyesho na muziki wa aina tofautitofauti.
Stephen Hawking akumbukwa
Pia kwenye sherehe hiyo zilitolewa heshima kwa mwanafizikia wa Uingereza na mhanga wa maradhi ya kulema kwa viungo vya mwili Stephen Hawking, aliefariki wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 76.
Hawking alieshiriki sherehe ya ufunguzi wa olimpiki ya walemavu mjini London mwaka 2012, alisifiwa na rais wa kamati ya kimataifa ya olimpiki ya walemavu Andrew Parsons katika hotuba yake ya kufunga michezo ya Pyeonchang, kama "hamasa" kwa watu wenye ulemavu.
Uwanja wa Olimpiki, uliogharimu dola milioni 80 kuujenga, sasa utavunjwa baada ya kujengwa tu kwa ajili ya sherehe za ufunguzi na ufungaji wa michezo yote. Michezo ijayo ya olimpiki ya walemavu itafanyika mjini Beijing mwaka 2022.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae
Mhariri: Sylvia Mwehozi.