1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Marekani yaonya kuhusu kampeni ya upotoshaji wa China

5 Oktoba 2023

Marekani imetahadharisha dhidi ya "kampeni ya kueneza taarifa za upotoshaji za China" inayoweza kudhoofisha amani na utulivu ulimwenguni.

Kituo cha Global Engagement Center cha Marekani kimetwikwa jukumu la kupambana na propaganda na upotoshaji.
Kituo cha Global Engagement Center cha Marekani kimetwikwa jukumu la kupambana na propaganda na upotoshaji.Picha: Kabinett des Präsidenten von Nord-Mazedonien

Machoni pa wengi ulimwenguni kote, China ina sifa mbaya kuhusu eneo lake la Xinjiang. Eneo la Xinjiang ni mahala ambapo watu wa jamii ndogo ya Uyghur wanafanyishwa kazi za kulazimishwa na kuwekwa kizuizini kiholela. Lakini kundi la waandishi habari wa kigeni waliozuru eneo hilo walikuwa na maoni tofauti kabisa.

Ziara hiyo ya mwezi Septemba ya waandishi habari 22 wa kigeni waliotangamana na jamii ya eneo hilo, ilifadhiliwa na China.

Baadaye waandishi hao wa habari waliliambia shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya China kwamba walifurahishwa na uchumi unaonawiri. Walieleza kwamba eneo hilo limejaa tamaduni, dini na makabila mbalimbali. Aidha walishutumu na kutengana na kile walichokiita uongo wa vyombo vya nchi za Magharibi.

Kwa namna gani China itaimarisha sera zake huko Xinjiang?

Ziara hiyo ni mfano wa kile Marekani inatizama kuwa ongezeko la juhudi za China kubadili mtizamo wa ulimwengu kuihusu. Inatumia mabilioni ya dola kila mwaka katika juhudi hizo.

Jinsi China yajaribu kubadili maoni ya umma

Katika ripoti yake ya kwanza kuhusu hilo, wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliainisha mbinu za China za kubadili maoni ya umma kama vile kufadhili taarifa potoshi, kutumia watu bandia kueneza uongo au kutumia ukandamizaji kuzima mtizamo wa kweli dhidi ya sifa zake.

Picha hii ya maktaba iliyopigwa Mei 31, 2019, inaonesha mnara wa ulinzi kwenye kituo chenye ulinzi mkali karibu na kile kinachoaminika kuwa kambi ya kuwaelimisha upya watu wa makabila madogo ya Kiislamu wanaozuiliwa viungani mwa Hotan, kaskazini magharibi mwa mkoa wa Xinjiang nchini China.Picha: Greg Baker/AFP

‘Global Engagement Center' kituo ambacho ni ni idara ya wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kilichotwikwa jukumu la kupambana na propaganda na upotoshaji, na ambacho kilitoa ripoti ya kurasa 58, kilitahadharisha kwamba kampeni ya upotoshaji ya China, hatimaye inaweza kushawishi jinsi maamuzi yanafanywa ulimwenguni kote na hata kudhoofisha masilahi ya Marekani.

China yakosoa ripoti kuhusu ukiukaji, Xinjiang

Katika kisa kimoja kilichoainishwa na ripoti hiyo ya Marekani, Serikali ya China iliunda mtoa maoni bandia anayeitwa Yi Fan, ambaye ripoti zake zinazopendelea Beijing zimeonekana katika majarida huko Asia, Afrika na Amerika ya Kusini.

Ripoti imeeleza kuwa katika mitandao ya kijamii, China inatumia vidude maalum vya kuongoza kampeni za kuzuia maudhui ya wakosoaji wa China huku zikikuza na kusambaza zile zinazosifu na kuunga mkono China. Imeongeza kuwa simu zilizotengenezwa China na kuuzwa nchi za nje, ziligunduliwa kuwekewa mfumo wa udhibiti.

Mkakati wa China kudhibiti idadi ya watu wa Xinjiang

Wanadiplomasia ni sehemu ya mpango wa China kujitakasa

Kando na waandishi habari, China pia imewapeleka wanadiplomasia Xinjiang katika safari za kupangwa kwa lengo la kujitakasa na kukabiliana na madai kwamba Beijing imewadhulumu kabila dogo la Uyghur la watu milioni 1.1 nchini humo kwa kuwaweka kizuizini kiholela, kuwafanyisha watu kazi kwa lazima katika viwanda vilivyo mbali na makazi yao.

Wakulima wakivuna pamba katika mji wa Hami, Xinjiang kaskazini magharibi mwaChina ambako wakaazi wake wengi ni Wauyghur.Picha: Pulati Niyazi/HPIC/dpa/picture alliance

Jamie Rubin, anayekiongoza kituo hicho amesema ikiwa hatua za China hazitadhibitiwa, basi uhuru wa kujieleza na kutoa maoni kinzani dhidi ya China unaweza kudidimizwa katika sehemu nyingi ulimwenguni.

Alisema Juhudi za Beijing zinaweza "kubadilisha mazingira ya habari ya kimataifa na kuharibu usalama na utulivu wa Marekani, wa marafiki, na wa washirika wake."

China: Marekani ndiyo chanzo cha upotoshaji na kitovu cha vita vya maoni

China ililaani ripoti hiyo na kuitaja yenyewe kuwa ni habari potoshi kwani haielezi ukweli uliopo. Kwenye jibu lake, wizara ya mambo ya Nje ya China imedai wizara nyenzake ya Marekani ndiyo chanzo cha upotoshaji na kitovu cha vita vya kimtizamo.

Kupitia taarifa, msemaji wa ubalozi wa China mjini Washington Lie Pengyu amesema ripoti hiyo ilikuwa kile alichokiita ‘chombo kingine cha kurudisha nyuma China na kuimarisha ubabe wa Marekani dhidi ya wengine.

Chanzo: APE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW