1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaonya kusambaa siasa kali Afrika

6 Agosti 2014

Rais Barack Obama anakutana na viongozi Afrika kuhitimisha siku tatu za mijadala juu ya usalama, nishati na utawala bora, huku Marekani ikionya kusambaa kwa siasa kali kwenye bara hilo linaloinukia kwa kasi kiuchumi.

Rais Barack Obama akihutubia kwenye Jukwaa la Biashara ya Afrika na Marekani mjini Washington tarehe 5 Agosti 2014, ikiwa ni sehemu ya mkutano kati ya pande hizo mbili.
Rais Barack Obama akihutubia kwenye Jukwaa la Biashara ya Afrika na Marekani mjini Washington tarehe 5 Agosti 2014, ikiwa ni sehemu ya mkutano kati ya pande hizo mbili.Picha: Reuters

Usiku wa jana (5 Agosti), Rais Obama aliwaalika marais wenzake zaidi ya 40 kutokea barani Afrika katika chakula cha usiku, alikojifaharishia pia kukutana na watu aliowaita kutoka bara la baba yake, ambalo alisema lina mustakabali mzuri wa ukuwaji wa uchumi.

"Tunyweni na tuleni kwa ajili ya Afrika mpya. Afrika ambayo inainuka na yenye matumaini tele, kwa ajili ya jukumu letu la pamoja la kuendelea kushirikiana kwa ajili ya amani na ustawi na haki inayosakwa na watu wetu na ambayo wanaistahiki kikamilifu," aliwaambia wageni hao wakati akiwakaribisha wageni wake kwenye chakula hicho katika Ikulu ya White House.

Obama alikumbushia kwamba kwake mkusanyiko huo ulikuwa na maana zaidi ya mkutano wa viongozi wakuu wa mataifa, kwani yeye ni mtoto wa baba wa Kiafrika kutokea Kenya na hilo ni sehemu muhimu ya historia familia yake. "Nimesimama mbele yenu kama rais wa Marekani na Mmarekani mwenye kujivunia nchi yangu. Nimesimama pia kama mtoto wa mwanamme mmoja kutoka Afrika. Damu ya Kiafrika inatembea kwenye familia yetu, na hivyo kwetu mafungamano kati ya nchi zetu, mabara yetu, ni ya kibinafsi zaidi."

Miongoni mwa waliohudhuria chakula hicho ni Rais Paul Kagame wa Rwanda, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Goodluck Jonathan wa Nigeria, Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini.

Marekani yaonya juu ya siasa kali Afrika

Hapo Jumatatu (4 Agosti), Zuma alimchokoza Rais Obama kwa kutofanya mengi kwa ajili ya Waafrika, licha ya asili yake ya Kikenya, lakini pia akasema anaelewa kwamba rais huyo wa Marekani anapaswa kuwa na tahadhari sana kutokana na kuwa na asili hiyo ya Kiafrika.

Mapema hapo jana, Rais Obama alitangaza mpango wa dola bilioni 33 wa uwekezaji barani Afrika, akisema kwamba Marekani inataka kuwa mshirika kwenye mafanikio ya bara hilo.

Baadhi ya viongozi wa Kiafrika wanaripotiwa kuamua kutohudhuria mkutano huo kwa sababu Obama hakutani nao kwa mazungumzo ya ana kwa ana. Badala yake, Makamu wake Joe Biden na waziri wake wa mambo ya nje, John Kerry, wamekuwa wakikutana kwenye vikao kadhaa na angalau viongozi wakuu wa nchi kumi, wakiwemo wa Afrika ya Kusini, Nigeria na Kenya.

Hapo jana, Kerry aliwaonya viongozi hao kwamba makundi ya siasa kali ni kitisho kikubwa kwa uchumi unaokuwa barani Afrika, kwani yanawalenga vijana wengi wasiokuwa na ajira.

Kerry alisema kwamba idadi ya watu milioni 700 wenye umri wa chini ya miaka 30 walioko Afrika, haijawahi kukutikana popote pale kwenye historia ya ulimwengu, na hivyo ni wajibu wa viongozi wa Afrika kulilinda kundi hilo lisiangukie mikononi mwa makundi kama vile Boko Haram la Nigeria na al-Shabaab la Somalia.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW