Marekani yaonywa
14 Agosti 2005Tehran:
Iran imemwonya Rais George W. Bush wa Marekani leo kuwa atafanya kosa kubwa iwapo atatumia nguvu dhidi ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu kwa ajili ya mradi wake wa kinuklia. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Iran, Hamid Reza Asefi, amesema kuwa Rais Bush anapaswa kufahamu kuwa uwezo wa Iran ni mkubwa zaidi kuliko ule wa Marekani. Wakati huo huo, Kansela Gerhard Schröder wa Ujerumani ameionya serikali ya Marekani kuhusu utumaiji wa nguvu dhidi ya Iran. Ameiomba Marekani ifikirie sana kile kinachotokea sasa hivi kutokana na vita vya Irak. Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani, Joschka Fischer, ametilia mkazo kwa kusema kuwa lazima juhudi za kidiplomasia ziendelezwe. Rais Bush ametishia kuwa haondoi uwezekano wa kutumia nguvu iwapo Iran itakataa kutekeleza miito ya kimataifa ya kusimamisha harakati zake za kinuklia.