Marekani yapeleka meli ya pili ya kivita Mashariki ya Kati
13 Februari 2026
Serikali ya Iran imetangaza siku ya Ijumaa kuanzishwa kwa tume ya uchunguzi. Tume hiyo itachunguza maafa ya maandamano yaliyoitishwa kupinga kupanda kwa gharama ya maisha ambayo yaligeuka na kuwa mikutano ya kuipinga serikali na vurugu hizo zikasababisha vifo vya maelfu ya watu.
Msemaji wa serikali ya Iran, Fatemeh Mohajerani, ameliambia shirika la habari la Iran (ISNA) kwamba ripoti ya mwisho itachapishwa hadharani baada ya kukamilika na hatua zaidi za kisheria baada ya mchakato huo zitatangazwa.
Maandamano hayo yalianza mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana na yaliongezeka zaidi ilipofika Januari 8. Zaidi ya watu 3,000 waliuawa, kulingana na hesabu rasmi. Mamlaka ya Iran imedai kwamba idadi kubwa ya waathiriwa walikuwa maafisa wa usalama na watu wa kawaida waliouawa na "magaidi" wanaozitumikia Israel na Marekani.
Hata hivyo, makundi ya kutetea haki za binadamu yaliyo nje ya Iran yanavishutumu vikosi vya usalama kwa kuwalenga waandamanaji.
Huku mvutano wa Iran na Marekani ukiwa unaendelea, kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesema meli kubwa zaidi ya kivita duniani, USS Gerald R. Ford, imeamriwa kusafiri kutoka Bahari ya Karibiki kwenda katika eneo la Mashariki ya Kati.
Hatua hiyo inafuatia wiki kadhaa za uimarishaji wa kijeshi wa Marekani katika Mashariki ya Kati, meli ya kwanza ya kivita kupelekwa ni USS Abraham Lincoln na meli hizo zinatarajiwa kuwepo katika eneo hilo hadi mwishoni mwa mwezi April au mapema mwezi Mei, jarida la New York Times limeripoti.
Rais wa Marekani Donald Trump anafikiria iwapo achukue hatua za kijeshi dhidi ya Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq Fuad Mohammed Hussein amesema nchi yake inapinga matumizi ya nguvu dhidi ya Iran. Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amezungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Saudi Arabia, mwanamfalme Faisal bin Farhan, siku ya Ijumaa. Mawaziri hao wawili walijadili hali ya Iran na mzozo wa Palestina na Israel.