1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yapinga azimio la UN la usitishaji mapigano Gaza

21 Novemba 2024

Marekani imepiga kura ya turufu jana kupinga azimio la Umoja wa Mataifa linalotoa wito wa kusitishwa mapigano kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, New York, Marekani
Mwakilishi wa Marekani alikosoa mpango huo kwa kutoungaisha usitishwaji mapigano na kuwachiwa kwa mateka wa IsraelPicha: Angela Weiss/AFP/Getty Images

Marekani ndio mwanachama pekee wa Baraza la Usalama aliyepiga kura ya kupinga mswada huo. Wanachama wengine 14 - wakiwemo washirika wa Marekani ambao ni Uingereza na Ufaransa - waliuunga mkono.

Soma pia: Wapalestina 15 wauawa na jeshi la Israel huko Gaza

Mwakilishi wa Marekani alikosoa mpango huo kwa kutoungaisha usitishwaji mapigano na kuwachiwa kwa mateka wa Israel. Rasimu hiyo iliyowasilishwa na wanachama 10 wasio wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama ilitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano na kuwachiliwa mara moja na bila mashariki kwa mateka wote ambao bado wanashikiliwa na Hamas.

Hata hivyo, haikuyaunganisha matukio hayo mawili. Balozi wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa alilitaja azimio hilo lililopendekezwa kuwa "la usaliti." Wakati huo huo, wizara ya Afya inayoendeleshwa na Hamas huko Gaza inesema idadi ya vifo katika ukanda huo inakaribia watu 44,000.