1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yapinga muhula wa tatu kwa Kagame

6 Juni 2015

Marekani itapinga hatua zozote zile za kumruhusu Rais Paul Kagame wa Rwanda kuwania muhula wa tatu wa urais baada ya mihula yake aliyoruhusiwa na katiba kumalizika hapo mwaka 2017.

Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Rais Paul Kagame wa Rwanda.Picha: Reuters

Mwanadiplomasia wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani ameliambia shirika la habari la AFP hapo Ijumaa (05.06.2015) kwamba "tumenuia kusaidia makabidhiano ya madaraka kwa amani kwa njia ya demokrasia kwa kiongozi mpya atakayechaguliwa na wananchi wa Rwanda."

Katiba ya Rwanda ya mwaka 2003 imeweka vikomo kwa mihula ya urais kuwa miwili na kwa hiyo inamzuwiya Kagame aliechaguliwa mara ya kwanza hapo mwaka 2003 na kuchaguliwa tena kwa kipindi cha pili hapo mwaka 2010 kuwania muhula wa tatu.

Lakini wiki iliopita maafisa wa serikali ya Rwanda wamesema bunge katika kipindi cha miezi miwili ijayo litajadili katika kikao chake mabadiliko ya katiba kwa kutilia maanani kile wafuasi wa Kagame walichokielezea kuwa ni "matakwa ya umma" yanayomtaka kiongozi huyo agombee tena urais.

Kukuza demokrasia

Serikali ya Marekani kwa muda mrefu imekuwa ikimuunga mkono Kagame mwenye umri wa miaka 57, kiongozi wa zamani wa waasi wa Kitutsi ambaye aliongoza shambulio lililokomesha mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 yaliofanywa na Wahutu wa misimamo mikali na baadae kuingoza nchi hiyo kuelekea kwenye ustawi wa kiuchumi.

Wananchi wa Rwanda katika harakati za uchaguzi mwaka 2010.Picha: picture-alliance/dpa

Lakini afisa huyo wa serikali ya Marekani ameweka wazi kwamba Mrekani haitounga mkono jaribio lolote lile la kuifanyia marekebisho katiba ili kuendelea kumbakisha madarakani mshirika wao huyo kupindukia muda uliopangwa kufanyika uchaguzi mpya nchini humo.

Amesema "Marekani inaamini kwamba demokrasia inakuwa imepiga hatua mbele kwa kujenga taasisi madhubuti na sio kuwa na mtu mwenye nguvu kubwa."

Ameongeza kusema kwamba kubadili katiba ili kuondowa muda wa muhula wa viongozi madarakani kwa kuwapendelea viongozi walioko madarakani hakwendani na misingi ya demokrasia na hupunguza imani kwa taasisi za kidemokrasia.

Msimamo wa Kagame

Maafisa wa serikali ya Rwanda wanakanusha kwamba Kagame mwenyewe binafsi anahusika na hatua hizo za kutaka kubadili katiba na imesisitiza kwamba imekuwa ikiitikia matakwa ya wananchi wengi wanaomuunga mkono Kagame.

Rais Paul Kagame wa Rwanda.Picha: Alexander Joe/AFP/GettyImages

Kagame ambaye muda wake wa uongozi unamalizika hapo mwaka 2017 amewahi kusema kwamba anapinga kuondolewa kwa kikomo cha mihula miwili lakini yuko tayari kubakia kwenye uongozi iwapo wananchi wataweza kumsadikisha akubali matakwa yao hayo.

Ibara nambari 101 ya katiba ya Rwanda inasema kwamba muhula wa miaka saba ya urais inaweza kuongezwa mara moja kwa muhula mwengine na "katika mazingira yoyote yale " mtu hapaswi kushikilia madaraka ya urais kwa zaidi ya mihula miwili.Wanasiasa kadhaa na watu wamesaini ombi la kutaka kufanyiwa marekebisho kwa katiba hiyo.

Vurugu za marekebisho ya katiba

Chama cha upinzani cha Kidemokrasia cha Kijani nchini Rwanda kimeitaka Mahakama Kuu kuliamuru bunge la Rwanda kutobadili ibara hiyo ya katiba nambari 101 na tayari kimewasilisha pingamizi mahakamani.

Machafuko ya Burundi.Picha: Reuters/G. Tomasevic

Hatua kama hizo za kutaka kubadili katiba zimezusha machafuko hivi karibuni katika nchi kadhaa za Kiafrika.

Mwaka jana rais wa zamani wa Burkina Faso Blaise Compaore alitimuliwa nchini humo kutokana na uasi wa umma baada ya kujaribu kurefusha muda wake madarakani kinyume na katiba.

Burundi nchi jirani na Rwanda imeingia kwenye machafuko kwa wiki kadhaa na kupelekea hata kuwepo jaribio la mapinduzi wakati Rais Piere Nkurunziza akijiandaa kuwania muhula wa tatu katika uchaguzi ambao unatajwa kuwa ni kinyume na katiba.

Mwandishi: Mohammed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri: Amina Abubakar