1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msaada wa dola bilioni 61 wapitishwa kwa Ukraine

Daniel Gakuba
24 Aprili 2024

Baraza la seneti la Marekani limepitisha muswada wa kitita cha dola bilioni 95 kwa ajili ya kuzisaidia kijeshi nchi washirika, sehemu kubwa ya msaada huo, dola bilioni 61 zikitengwa kwa ajili ya Ukraine.

USA, Washington | Bendera za Marekani na Ukraine
Baraza la seneti la Marekani limepitisha muswada wa kitita cha dola bilioni 95 kwa ajili ya kuzisaidia kijeshi nchi washirika.Picha: Nathan Howard/Getty Images

Muswada huo wa msaada wa kijeshi kwa Ukraine na washirika wengine wa Marekani, Israel na Taiwan, ulitarajiwa kupita kirahisi katika baraza la seneti, baada ya kukwama katika Baraza la Wawakilishi katika muda wa miezi sita.

Akizungumza mara tu baada ya Baraza la Seneti kuupitisha muswada huo kwa kura 79 dhid ya 18, Rais Joe Biden amesema na hapa nanukuu, ''usiku huu maseneta wengi kutoka vyama vyote viwili wameungana na Baraza la Wawakilishi kuitikia mwito wa kihistoria katika wakati huu muhimu.'' Mwisho wa kunukuu.

Aidha, Biden amesema atautia saini kuwa sheria mara tu utakapofika mezani kwake, na baadaye atawahutubia wananchi wa Marekani.

Ukraine yaishukuru Marekani kwa msaada wa Kijeshi

Hatua hiyo ya baraza la seneti la Marekani imepokelewa kwa shangwe nchini Ukraine. Rais wa nchi hiyo Volodymyr Zelenskiy kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X azamani ukijulikana kama twitter, amewashukuru viongozi wa vyama viwili, Chuck Schumer wa Wademokrati walio wengi na Mitch McConnell wa Warepublikan walio wachache, kwa alichokielezea kama uongozi mahiri uliowezesha muswada huo kupitishwa.

Ukraine yasema msaada wa Marekani ulikuwa unasubiriwa kwa shauku kubwa 

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akiwa na mwenzake wa Marekani Joe Biden Picha: CHIP SOMODEVILLA/AFP/Getty Images

Hali kadhalika, Yuriy Sak ambaye ni mshauri katika wizara ya masuala ya kimkakati ya Ukraine, amesema msaada huo wa Marekani umekuwa ukisubiriwa kwa shauku kubwa. Katika mazungumzo na DW, afisa huyo amesema walikuwa wanaishiwa na risasi na mizinga, na makombora yanayotumiwa na mifumo ya ulinzi wa anga.

Sak amesema uamuzi huu uliopitishwa mjini Washington utaongeza uwezo wa Ukraine kujibu mashambulizi ya adui wao, na kupeleka ujumbe wa matumaini kwa wanajeshi walioko msitari wa mbele wa mapigano.

Bunge la Marekani kupigia kura miswada ya msaada

Katika mahojiano na televisheni ya DW, mtaalamu wa masuala ya kijeshi kutoka Chuo Kikuu cha King's College mjini London, Mike Martin, amesema msaada huu wa Marekani ni mkubwa kuliko fedha zote ambayzo Marekani imeipatia Ukraine kuanzia mwaka 2022 hadi leo, na kwamba ni kiasi ambacho hakijawahi kuonekana tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Martin amesema ingawa bado ni mapema kuzungumzia hali ya kubadili wizani wa vita hivyo ambao umekuwa ukilalia upande wa Urusi mnamo miezi ya hivi karibuni, msaada huu unaipa Ukraine kigezo ambacho ilikuwa ikikosa kuweza kufanikiwa. Amesema tayari Ukraine inayo ari, na imeboresha utaratibu wake wa kuwasajili wapiganaji, na sasa, inapatiwa nyenzo na vifaa kukamilisha matakwa ya kuendesha vita kwa ufanisi.

Vyanzo: mk/fb (AP, Reuters)