1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yarejesha mazungumzo ya ulinzi na Urusi

Sylvia Mwehozi
22 Oktoba 2022

Mawaziri wa ulinzi wa Marekani na Urusi Lloyd Austin na Sergei Shoigu wamefanya mazungumzo siku ya Ijumaa kwa njia ya simu ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwezi Mei.

USA Verteidigungsminister Lloyd Austin
Picha: Kevin Wolf/AP Photo/picture alliance

Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin, "amesisitiza juu ya umuhimu wa kuendeleza mawasiliano katikati mwa vita vinavyoendelea nchini Ukraine" wakati wa mazungumzo yake kwa njia ya simu na mwenzake wa Urusi Sergei Shoigu. Wizara ya ulinzi ya Urusi imethibitsiha mazungumzo hayo ikisema wakuu hao wamegusia suala la Ukraine bila ya kutoa maelezo zaidi.

Mara ya mwisho mawaziri hao kufanya mazungumzo ilikuwa ni Mei 13 wakati Austin alipoitolea mwito Moscow kutekeleza usitishaji wa haraka wa mapigano nchini Ukraine. Austin: Ukraine inaweza kuishinda Urusi

Aidha, Austin alifanya mazungumzo tofauti na waziri mwenzake wa Ukraine Oleksiy Reznikov "kusisitiza dhamira isiyoyumba ya Marekani ya kuunga mkono uwezo wa Ukraine wa kukabiliana na uchokozi wa Urusi" .

Lakini waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amesema kuwa haoni dhamira ya dhati kutoka kwa Urusi juu ya mazungumzo mapana ya kumaliza vita vya Ukraine. Blinken amesisitiza kwamba Washington itaendeleza mawasiliano na Urusi lakini juhudi pana za kidiplomasia zinategemea na utashi wa rais Vladimir Putin wa "kukomesha uchokozi".

Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei ShoiguPicha: Russian Defence Ministry/REUTERS

"Hatujaona ushahidi wa hilo kwa wakati huu. Kinyume chake, tunaona uchokozi wa Urusi ukiongezeka maradufu," Blinken aliueleza mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari na waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Catherine Colonna.

Ameongeza kuwa "tofauti ya kimsingi ni kwamba Waukraine wanapigania nchi yao, ardhi yao, mustakabali wao. Urusi haipiganii hilo na ikiwa Rais Putin ataelewa hilo kwa haraka na kufikia hitimisho hilo, ndivyo tutaweza kumaliza vita hivi mapema."

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani, alikutana na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov mnamo mwezi Januari kuonya juu ya matokeo ya uvamizi, ambao Moscow iliendelea nao mwezi mmoja baadaye. Tangu wakati huo Blinken amekataa kuonana na Lavrov lakini alizungumza naye kwa njia ya simu mwezi Julai katika jitihada za kuwaachilia Wamarekani waliofungwa nchini Urusi.

Rais Joe Biden na Rais Vladmir Putin wote wameondoa matumaini ya mazungumzo ya mwezi ujao kando ya mkutano wa kilele wa kundi la nchi 20 zilizopiga hatua kiviwanda huko Bali Indonesia.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW