1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Marekani yasaka njia mpya kutekeleza vikwazo kwa Pyonyang

15 Aprili 2024

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas Greenfield, amesema nchi yake na washirika wake wanatafuta njia mpya ya kutekeleza vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield.Picha: Angela Weiss/AFP

Hilo linafuatia wasiwasi uliopo kwamba Pyongyang bado inaendelea na mpango wake wa silaha za nyuklia.

Nate Evans, msemaji wa Ujumbe wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesema Thomas-Greenfield ambaye yuko mjini Seoul ataitembelea pia Japan kuendeleza ushirikiano kwa vikwazo hivyo.

Baada ya mkutano wake na rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol na waziri wa mambo ya nchi za nje wa taifa hilo Cho Tae-yul, Thomas-Greenfield  amesema anaunga mkono juhudi za Korea Kusini za kusambaratisha mpango wa Korea Kaskazini na kuimarisha uwepo wa haki katika eneo lililojitenga.

Mwezi uliopita Urusi ilitumia kura yake ya turufu kupinga kurefushwa muda wa jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaofuatilia vikwazo vya kimataifa vilivyodumu kwa miaka 15 dhidi ya Korea Kaskazini kutokana na mipango yake hiyo ya silaha za nyuklia.

Korea Kaskazini imekuwa ikishikilia msimamo wake kwamba mpango wake wa nyuklia ni kwaajili ya ulinzi ya vitisho vya nje kama Marekani na Korea Kusini na kusema vikwazo dhidi yake ni sawa na ukiukwaji wa uhuru wake.