1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani Yasalimika na Mgogoro wa Fedha

2 Januari 2013

Mvutano wa bajeti ya Marekani, mwaka wa uchaguzi mkuu nchini Ujerumani na mazungumzo pamoja na kiongozi wa waasi wa kikurdi nchini Uturuki, ni miongoni mwa mada zilizohanikiza katika magazeti ya Ujerumani.

Rais wa Marekani Barack Obama na makamo wake Joe BidenPicha: Reuters

Tunaanzia Marekani ambako baraza la wawakilishi limefuata nyayo za baraza la Seneti na kuunga mkono mswaada wa sheria kuiepushia Marekani balaa la kutumbukia katika mgogoro wa kiuchumi. Hata hivyo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanahisi vyama vya kisiasa nchini Marekani vinatanguliza mbele masilahi yao badala ya yale ya taifa. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaandika:"Kwa mara nyengine tena pande zinazozozana zimefikia makubaliano ya dakika ya mwisho, kama ilivyotokea mwishoni mwa mwaka 2010 katika mzozo wa kupunguza makali ya kodi za mapato na msimu wa kiangazi mwaka 2011 ulipozuka mvutano kuhusu kiwango cha juu cha madeni ya serikali. Lakini desturi hizo zinazofuatwa kila mwaka kukiuka muda uliowekwa na kufikia makubaliano usiku wa manane zimewachosha wananchi. Kasheshe hiyo ya kisiasa inafuja hadhi ya nchi hiyo tangu ndani mpaka nje. Jamii imeingiwa na kero na kughadhibika kwa sababu wanahisi viongozi wa mjini Washington wanashindwa kuipatia ufumbuzi migogoro mikubwa inayoikaba nchi hiyo ambayo ni pamoja na madeni, nakisi ya bajeti, ukosefu wa ajira, mzozo katika sekta ya elimu na miundo mbinu iliyopitwa na wakati, gharama zilizokithiri katika sekta ya afya na huduma za uzeeni.

Mwaka wa Uchaguzi Ujerumani

Waziri mkuu wa jimbo la Lower Saxony David McAllisterPicha: dapd

Mada ya pili magazetini hii leo inahusiana na pirika pirika kuelekea mwaka wa uchaguzi nchini Ujerumani. Tangu mwaka jana utafiti wa maoni ya wananchi unaashiria yasiyo ya kuvutia kwa baadhi ya vyama vidogo vidogo vya kisiasa. Gazeti la Westfalen-Blatt linaandika:"Chama cha FDP kikishindwa katika uchaguzi wa bunge katika jimbo la Lower Saxony, mapema mwaka huu, itakayoathirika sio pekee serikali ya muungano ya vyama vya CDU na waliberali inayoongozwa na waziri mkuu, David McAllister. Kwa sababu Hannover, sawa na Berlin inaangaliwa kuwa ni sawa na wizani kwa uchaguzi mkuu wa msimu wa mapukutiko kwa chama cha CDU. Na Social Democratic na walinzi wa mazingira die Grüne, hawajijui baada ya mgombea wa SPD, Peer Steinbrück, mara kwa mara akijikwaa katika suala la fedha, kwa namna ambayo pengine muungano pamoja na kansela anayezidi kupata nguvu hautaweza kuepukwa.

Mazungumzo ya Amani Uturuki

Waziri mkuu wa Uturuki Tayyip ErdoganPicha: Reuters

Ripoti ya mwisho inahusiana na mazungumzo kati ya serikali ya Uturuki na kiongozi wa chama cha waasi wa kikurdi,PKK, Abdullah Öcalan. Gazeti la Berliner Zeitung linaandika."Waziri mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan, ameruhusu mazungumzo ya amani pamoja na kiongozi wa PKK aliyeko kizuwizini, Abdullah Öcalan. Berliner Zeitung linasema serikali ya Uturuki imetambua hatimaye bila ya "adui huyo mkubwa wa taifa" hakuna ufumbuzi unaoweza kupatikana kumaliza mzozo wa mtutu wa bunduki wa Wakurdi."

Mwandishi:Hamidou Oummilkher/Inlandspresse

Mhariri:Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW