1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nikki Haley asema Afrika ni bara muhimu kwa Marekani

Yusra Buwayhid
19 Januari 2018

Mabalozi wa nchi za Afrika katika Umoja wa Mataifa wamemtaka Rais wa Marekani Donald Trump akutane na viongozi wa Kiafrika katika mkutano wa kilele Ethiopia baada ya kuripotiwa kutoa matamshi machafu dhidi ya bara hilo.

Nikki Haley
Picha: picture-alliance/M.Altaffer

Wito huo umetolewa katika mkutano wa faragha na balozi wa Marekani Nikki Haley mjini New York. Haley amewaambia mabalozi hao kwamba Afrika ni muhimu kwa Marekani, lakini hakuomba msamaha kwa niaba ya Rais Donald Trump aliyedaiwa kutoa matamshi machafu dhidi ya bara hilo.

Balozi wa Guinea ya Ikweta kwenye Umoja wa Mataifa, Anatolio Ndong Mba, amewaambia waandishi habari baada ya mkutano huo wa faragha ulioitishwa na Haley, kwamba wanatarajia  viongozi wa mataifa ya Afrika kuombwa radhi na pengine kutoka kwa Trump wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika utakaofanyika mjini Addis Ababa Ethiopia Januaria 28 hadi 29.

Ndong Mba amesema kundi hilo la mataifa 54 ya Afrika katika Umoja wa Mataifa limempa Haley kile alichokijata kama pendekezo maalaum bila kulitolea ufafanuzi zaidi.

Wanadiplomasia wengine, waliozungumza bila ya kutaka kutajwa kwa majina kwa vile hawakuwa na mamlaka ya kuzungumza hadharani, wamesema pendekezo hilo lililikuwa ni kumtakaTrump kutuma ujumbe kwa viongozi wa Kiafrika katika mkutano huo.

Mkutano wa Umoja wa Afrika huko Addis Ababa, EthiopiaPicha: picture alliance/AA/M. Wondimu Hailu

Trump aliyataja mataifa ya barani Afrika kuwa ni nchi za uvundo wiki iliyopita wakati akikataa pendekezo linalohusu uhamiaji. Rais huyo hata hivyo baadae alikanusha kutumia lugha hiyo.

Ijumaa iliyopita  kundi hilo la Wanadiplomasia wa Kiafrika lilitoa taarifa ya kulaani matamshi hayo lililoyataja kuwa ni machafu, ya kibaguzi na yenayoonesha chuki dhidi ya wageni, na kumtaka Trump aombe msamaha.

Haley alimwambia Ndong Mba kwamba yeye hakuwapo katika mkutano huo na hana uhakika wa alichokisema Trump, lakini alimueleza kwamba rais wa Marekani siku zote amekuwa akilizungumzia vyema bara la Afrika. Ndong Mba amesema Haley amesikitishwa sana na yote yaliyotokea na ameuelezea mkutano baina yao kama wa kirafiki na uliokuwa na uwazi.

Umoja wa Afrika  wenye nchi wanachama 55, pamoja na mataifa kadhaa ya Kiafrika binafsi yalishtushwa na matamshi hayo ya Trump na kuyalaani.

Ndong Mba amesema waliridhishwa na uamuzi wa Haley wa kukutana nao, na wakazungumzia ushirikiano kati ya Marekani na Afrika.

Kabla ya hata Trump kutoa matamshi hayo machafu, wasiwasi juu ya uongozi wake umekuwa ukiongezeka barani Afrika, bara la pili kwa ukubwa wa idadi ya watu duniani.

Bara hilo limekuwa likiulalamika utawala wa Trump kwa kupunguzwa kwa kiwango cha msaada wa  Marekani pamoja na kupotea kwa lengo la ushirikiano wa kupambana na makundi yenye misimamo mikali barani humo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/ap

Mhariri: Daniel Gakuba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW