Marekani yasema Assad asiwe katika serikali ya mpito
9 Mei 2013Akizungumza mjini Roma baada ya kukutana na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Jordan Nasser Judeh, John Kerry amesema kuwa wadau wote katika juhudi za kutafuta amani nchini Syria, wanashughulikia kuundwa kwa serikali ya mpito itakayokubaliwa na pande zinazohasimiana nchini humo. Hata hivyo, waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani amesisitiza kuwa kwa maoni yao, rais Bashar al-Assad hapaswi kuhusika katika serikali hiyo. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekubaliana na maoni hayo ya John Kerry.
''Sisi pia maoni yetu ni kwamba Bashar al-Assad amepoteza uhalali wa kuwa kiongozi. Lakini pia tunafahamu kuwa tunalo jukumu la kuweka mchakato utakaowezesha kufanikisha kipindi chote cha mpito.'' Amesema kansela Merkel.
Muafaka wa kimataifa
Kerry pia alisema mchakato wa kufanyika kwa mkutano wa kimataifa kuhusu Syria ulikuwa ukiendelea, baada ya kukubaliana na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov kwamba nchi zao zitashirikiana katika suala hilo. Alisema alizungumza na mawaziri wa nchi za nje wa mataifa yote yanayohusika katika mkutano huo, na kuongeza kuwa mawaziri wote hao waliukaribisha mkutano huo, na kuelezea utashi wao kushiriki katika juhudi zote za kumalizia vita vya Syria kwa njia ya mazungumzo.
Aidha, John Kerry alisema amewasiliana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, na kuongeza kuwa pande zote zinazohusika zitafanya hima kuuandaa mkutano huo. Mkutano huo wa kimataifa kuhusu Syria unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu wa Mei, ingawa mahali utakapofanyika bado hapajaamuliwa.
Katika juhudi hizo hizo za kutafuta suluhu kwa mzozo wa Syria, Rais wa Marekani Barack Obama atakutana na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron mjini Washington Jumatatu ijayo, kuzungumzia suala hilo. Viongozi hao pia watakutana tena kwenye mkutano wa nchi nane zinazoongoza kiviwanda, utakaofanyika mwezi ujao huko Ireland ya Kaskazini.
Kabla ya kwenda Marekani, Cameron atafanya mazungumzo na rais wa Urusi Vladimir Putin Ijumaa wiki hii. Cameron amesema mazungumzo yake na Putin yatahusu kile alichokiita ''hatua za dharura'' kuelekea kipindi cha mpito kitakachomaliza umwagaji damu nchini Syria.
Al-Nusra yakanusha
Nchini Syria kwenyewe, kundi lenye nguvu la al-Nusra lenye msimamo mkali wa kiislamu, limekanusha taarifa kuwa kiongozi wake Abu Mohammed al-Jawlani amejeruhiwa kwenye uwanja wa mapambano karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Damascus. Kamanda wa kundi hilo al-Ghareeb al-Muhajir al-Qahtani amesema kuwa taarifa hizo zilizotangazwa na vyombo vya habari ni uongo wa serikali ya rais Bashar al-Assad.
Kujeruhiwa kwake pia kulitangazwa na shirika linalochunguza haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza, ambalo lilisema kuwa alipata jeraha mguuni.
Kundi la al-Nusra, mwezi uliopita lilitangaza utiifu wake kwa kiongozi wa mtandao wa al-Qaida Ayman al-Zawahri, na kuthibitisha kile ambacho kilikuwa kikishukiwa kuwa baadhi ya makundi ya waasi wa Syria yalikuwa na mafungamano na mitandao ya kigaidi.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/RTRE
Mhariri:Yusuf Saumu