1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Marekani yasema kamwe haitoiacha Ukraine ishindwe

19 Machi 2024

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin ameiahidi Ukraine kwamba itaendelea kuungwa mkono kimataifa katika juhudi zake za kujilinda dhidi ya uvamizi wa Urusi.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd AustinPicha: Daniel Roland/AFP/Getty Images

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kimataifa kuhusu Ukraine unaofanyika katika Kambi ya Kikosi cha jeshi la anga la Marekani huko Ramstein, nchini Ujerumani, Austin amesema ujumbe wao uko wazi na kwamba Marekani haitoiacha Ukraine ishindwe, hata ikiwa Baraza la Congress limezuia msaada zaidi wa dola bilioni 60 kwa ajili ya Ukraine na wakati ambapo vikosi vya Kiev vinakabiliwa na uhaba wa silaha.

Soma zaidi: Marekani kuichangia Ukraine dola milioni 300 

Aidha, Marekani imeonya kuwa msaada wa hivi karibuni wa dola milioni 300 utadumu kwa wiki chache tu.

''Hii ni hatua muhimu na isiyo ya kawaida ya kusaidia mahitaji muhimu zaidi ya Ukraine ya ulinzi wa anga, silaha na mifumo ya kuzuia makombora. Lakini bado tumeazimia kuipatia Ukraine rasilimali ambazo inazihitaji kupambana na uchokozi wa Ikulu ya Urusi ya Kremlin," alisisitiza Austin.

Mawaziri wa ulinzi wa Ujerumani, Marekani na Ukraine wakiwa kwenye mkutano Ramstein, UjerumaniPicha: Michael Probst/AP/picture alliance

Hata hivyo, Ukraine imesema inashangazwa na kushtushwa kuona kuwa Marekani bado haijaidhinisha msaada mpya, wakati ambapo inakabiliwa na uhaba wa silaha katika uwanja wa mapambano miaka miwili tangu Urusi ilipoivamia nchi hiyo.

Akizungumza na vyombo vya habari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Dmytro Kuleba amesema wanakaribia kufikia mwishoni mwa mwezi Machi na majadiliano yanaendelea, majadiliano kuhusu masuala ya maslahi muhimu, maslahi ya kimkakati ya Marekani barani Ulaya.

Zelensky asema msaada wa Marekani ni muhimu

Matamshi hayo ameyatoa siku moja baada ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kusema kuwa uamuzi wa haraka kutoka kwenye bunge la Marekani ulikuwa muhimu. Aliyasema hayo wakati wa mkutano wake na Seneta wa Marekani, Lindsey Graham.

Majeshi ya Ukraine yameripoti kuwepo kwa uhaba wa silaha kutokana na kuchelewa kwa msaada, huku vikosi vya Urusi vikizidi kusonga mbele kwenye maeneo ya mapambano.

Askari wa Ukraine wakiwa Avdiivka, mashariki mwa UkrainePicha: Narciso Contreras/Anadolu/picture alliance

Wakati huo huo, Rais wa Urusi, Vladmir Putin ameitaka Idara ya Usalama ya Shirikisho la Urusi, FSB, kuwatambua na kuwaadhibu wapiganaji wa Urusi wanaoiunga mkono Ukraine, ambao wameshiriki katika mashambulizi kadhaa yanayoongezeka kwenye maeneo ya mipakani na kusababisha vifo. Putin amesema wasaliti hao lazima watambuliwe kwa majina yao, na waadhibiwe popote pale walipo.

Ama kwa upande mwingine, mkuu wa idara ya ujasusi ya kigeni wa Urusi, Sergei Naryshkin amesema Jumnne kuwa jeshi lolote la Ufaransa litakalopelekwa Ukraine kusaidia kupambana na Urusi litakuwa shabaha ya kipaumbele na halali kwa mashambulizi yatakayofanywa na vikosi vya Urusi.

Na katika uwanja wa mapambano, Urusi imesema kuwa vikosi vyake vimechukua udhibiti wa kijiji cha Orlivka kilichopo umbali wa kilomita 4 magharibi mwa jimbo la Avdiivka, mashariki mwa Ukraine.

(AFP, DPA, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW